SHINYANGA: MASHINDANO YA MBIO ZA BAISKELI YAFANA, WASHINDI WAJINYAKULIA ZAWADI KUBWA

Mdhamini wa mashindano hayo ya mbio za baiskeli, Mkurugenzi wa CM Entertainment, Bwana Clouds Malunde, akimkabidhi ufunguo wa Pikipiki ambayo ni zawadi yake baada ya kuwa  mshindi wa kwanza kundi A katika mbio za Baskeli Mkoa wa Shinyanga leo Agosti 8,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mashindano ya mbio za baiskeli yamefana leo, Agosti 8, 2024, katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, ambapo washindi wamepokea zawadi mbalimbali, ikiwemo pikipiki aina ya SANLG, Ng’ombe, pamoja na fedha taslimu na kwamba Mashindano hayo yamedhaminiwa na CM Entertainment.

Katika mashindano hayo, makundi mbalimbali yalishiriki kushindania zawadi hizo, yakiwemo kundi la wanawake, ambao walikimbia huku wamebeba ndoo za maji kichwani, kundi la wazee, pamoja na makundi ya vijana, ikiwemo kundi D, kundi C, kundi B, na kundi A Makundi haya yalizunguka laundi mbalimbali, ikiwemo laundi 50, laundi 100, na laundi 150 kwa kundi la mwisho.

Washindi wa makundi yote wamepatiwa zawadi zao ambapo kwa kundi A, mshindi wa kwanza alikuwa George Zengo Ndimila mkazi wa Samuye ambaye amejinyakulia Pikipiki mpya aina ya SANLG, Mshindi wa pili amepewa zawadi ya shilingi milioni moja, huku mshindi wa tatu akipokea shilingi laki nane.

Mdhamini wa mashindano hayo ya mbio za baiskeli, Mkurugenzi wa CM Entertainment, Bwana Clouds Malunde, amewapongeza washindi wote waliopokea zawadi zao leo, huku akiwatia moyo wasikate tamaa na waendelee kutetea nafasi zao ili wawe washindani wa kitaifa na kimataifa.

“Natoa pongezi na shukurani kwa washindi wetu wote, hususan mshindi wa kwanza kutoka kundi A, Bwana George Zengo Ndimila, ambaye amejinyakulia pikipiki mpya aina ya SANLG kutoka kwangu, muandaaji na Mkurugenzi wa CM Entertainment, Nampongeza kwa juhudi na mazoezi yake ya muda mrefu; amejituma hadi kufikia malengo na ndoto zake za kumiliki pikipiki,” amesema Malunde.

Bwana Malunde ametoa wito kwa wale ambao wanatamani kuingia kwenye mashindano ya baiskeli, akiwakaribisha na kuwasisitiza waendelee kufanya mazoezi na kujifunza kila siku ili waweze kufikia malengo yao.

“Mimi kama muandaaji, bado ninaendelea kufanya vitu vikubwa kuhakikisha wanaokimbia mbio za baiskeli tunawabadilishia maisha yao kuwa mazuri zaidi. Ahadi yangu ni kwamba mwaka kesho tutakuwa na mashindano yanayoitwa ‘JENGA NA MBIO ZA BAISKELI KWA CM ENTERTAINMENT’, ambapo mshindi wa kwanza atapewa mifuko ya simenti, mabati, na vitu vingine ili akamilishe ujenzi wa nyumba yake,” .ameongeza Malunde.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Waendesha Baiskeli Mkoa wa Shinyanga, Bwana Kasi Salula, amesema kuwa zaidi ya watu elfu tano (5000) wako kwenye makundi ya waendesha baiskeli mkoani Shinyanga ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali wa michezo, ikiwemo serikali, kuunga mkono jitihada za vijana hao ili waweze kunufaika na mchezo wa mbio za baiskeli.

Baadhi ya waendesha baiskeli walioshiriki michezo hiyo leo wamemshukuru Mkurugenzi wa CM Entertainment, Bwana Clouds Malunde, kwa udhamini wake, ambao umewasaidia kupata zawadi mbalimbali zitakazowasaidia kujikwamua kimaisha.

Waendesha baiskeli hao wamesema kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya baiskeli na miundombinu bora.

Wameiomba serikali ya Mkoa wa Shinyanga kuwaunga mkono kwa kutengeneza miundombinu bora, ili mchezo huu uwe sehemu ya kutengeneza ajira kwa vijana.

Mashindano ya mbio za baiskeli kwa mwaka huu 2024 yamefanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage kama sehemu ya maadhimisho ya sikukuu ya Wakulima (Nanenane), ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Agosti 8.

Awali kundi la wanawake wakijiandaa kuzunguka wakiwa wamebeba ndoo za maji kichwaji.


 

TAZAMA VIDEO


Previous Post Next Post