Na Mapuli Kitina Misalaba
Tamasha la Sanjo ya Busiya (77Fest) 2024, lililofanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 1 hadi 7 Julai, limehitimishwa kwa mafanikio makubwa na shukrani tele kutoka kwa viongozi na washiriki. Tamasha hili lenye lengo la kuenzi na kusherehekea utamaduni na umoja wa Wana Busiya, lilivutia hadhira ya takriban watu 40,000 kutoka ndani na nje ya Utemi wa Busiya.
Mgeni wa heshima katika tamasha hilo alikuwa Dr. Augustus Kyalo Muli, Chifu kutoka jamii ya Anzuani huko Kitui, Kenya. Dr. Muli aliongozana na viongozi wengine watano pamoja na wachezaji ngoma wa kikundi cha Itumani. Katika hotuba yake, aliwapongeza waandaaji wa tamasha kwa juhudi zao za kuendeleza mila na desturi za Wasukuma, akisisitiza umuhimu wa kuwarithisha vijana utamaduni ili wawe na maadili mema.
Mbali na Chifu Muli, viongozi wengine wa kimila walioshiriki ni pamoja na Chifu Josephat Nkingwa Kiseni II kutoka Himaya ya Busumabu, Chifu Aron Mikomangwa Nyamilonda III kutoka Himaya ya Mwanza, na Chifu Charles Doto Balele Itale kutoka Himaya ya Bujashi. Viongozi hawa walionyesha mshikamano wao na kupongeza juhudi za Wana Busiya katika kuhifadhi utamaduni wao.
Siku ya hitimisho la tamasha, viongozi mbalimbali wa serikali walihudhuria, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ambaye aliwahakikishia waandaaji kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono katika kuendeleza mila na desturi za Mtanzania.
Chifu Edward Makwaia, Ntemi wa Busiya, alitoa shukrani za dhati kwa viongozi wote wa kimila, serikali, na wananchi waliofanikisha tamasha hili. Alisisitiza kuwa tamasha hili limeendelea kuwa kubwa na kwamba mwaka 2025, Sanjo ya Busiya itakuwa na hamasa zaidi. Alimaliza kwa kuwaalika Wana Busiya kushiriki kwa wingi na kuchangia katika maandalizi ya tamasha lijalo.