Na Mapuli Kitina Misalaba
Tamasha la Sabasaba linalofahamika kama Sanjo
ya Busiya, ambalo huandaliwa na ikulu ya Chifu (Mtemi) Makwaiya, kila Mwaka
ifikapo Mwezi Julai huko Ukenyenge Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga.
Tamasha hili
la Sanjo ya Busiya (77Fest) 2024, ambalo hufanyika kwa siku saba kuanzia tarehe
1 hadi 7 Julai, ikiwa lengo ni kuenzi na
kusherehekea utamaduni na umoja wa Wana Busiya,.
Zaidi ya watu 40,000 hujitokeza kutoka ndani na nje ya Utemi
wa Busiya ambapo Tamasha hili, lina lengo la kuendeleza
na kuhifadhi mila na desturi za kabila la Wasukuma na kwamba tamasha hili
linatoa fursa kwa wananchi kushiriki katika ngoma za asili na kufurahia vyakula
vya asili, hivyo kusaidia kuendeleza utamaduni wa Wasukuma.
Mgeni Rasmi na Hotuba Yake
Mgeni rasmi katika tamasha la mwaka huu
alikuwa Dkt. Augustus Muli, Kaunti ya Kitui kutoka kabila la Wakamba nchini
Kenya. Dkt. Muli aliwapongeza waandaaji wa tamasha kwa juhudi zao za kuendeleza
mila na desturi za kabila la Wasukuma ambapo alisema kuwa kuenzi mila na
desturi ni muhimu ili kuwarithisha vijana maadili mema na kuzuia mmomonyoko wa
maadili.
"Tunafurahi kualikwa kwenye tamasha hili
la Sanjo ya Busiya na Chief Edward Makwaiya na kuona utamaduni wa Kisukuma.
Sisi Wakamba na Wasukuma ni ndugu sasa tulioana na majina yetu yanaingiliana.
Tutakuja kuwaalika pia mje Kenya," alisema Dkt. Muli.
Dkt. Muli pamoja na mambo mengine aliipongeza
serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono masuala ya utamaduni.
Hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi
Macha, alisema kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono viongozi wa kimila
katika juhudi zao za kuendeleza na kuhifadhi mila na desturi za Mtanzania huku
akisisitiza kuwa serikali haina ukabila lakini inatambua na kuheshimu makabila
mbalimbali nchini.
"Serikali haina ukabila, lakini ina
makabila mbalimbali ambapo wananchi huenzi mila na desturi zao," alisema Mhe. Macha.
RC Macha aliwataka machifu kuweka kando mila
potofu na kuenzi mila nzuri ambazo zinaweza kurithishwa kwa vijana ili kuzuia
mmomonyoko wa maadili.
Ujumbe kwa Viongozi wa Kimila
Mhe. Macha pia alitumia nafasi hiyo
kuwakumbusha viongozi wa kimila kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu
katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Kwa upande wake, Mtemi wa himaya ya Busiya,
Edward Makwaiya, aliahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika juhudi za
kulinda na kuendeleza mila na desturi za wakazi wa eneo hilo.
Chifu
Edward Makwaia, Ntemi wa Busiya, alitoa shukrani za dhati kwa viongozi wote wa
kimila, serikali, na wananchi waliofanikisha tamasha hili huku akisisitiza kuwa
tamasha hilo limeendelea kuwa kubwa na kwamba mwaka 2025, Sanjo ya Busiya itakuwa
na hamasa zaidi ambapo alimaliza kwa kuwaalika Wana Busiya kushiriki kwa wingi
na kuchangia katika maandalizi ya tamasha lijalo.
Pongezi za Mbunge wa Kishapu
Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Boniphace
Butondo, alilipongeza tamasha hilo la utamaduni kwa kuwaunganisha Wasukuma na
kuenzi tamaduni zao huku akiahidi kuendelea kuwaunga mkono waandaaji wa tamasha
hilo ili kufikia malengo yao katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Maoni ya Wananchi
Baadhi ya wananchi waliohudhuria tamasha hilo
walieleza furaha yao na kuomba tamasha hilo liendelezwe zaidi ambapo walisema
kuwa tamasha hilo ni fursa muhimu ya kujifunza mambo mbalimbali ya mila na
desturi kupitia elimu inayotolewa.
Washiriki wa Tamasha
Tamasha hili lilihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali, taasisi binafsi, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama
vya siasa, wadau, na wananchi.
Wasanii wa ngoma za asili kutoka kabila la
Wasukuma na Wakamba waliburudisha katika tamasha hilo.
Viongozi wa Kimila
Baadhi ya viongozi wa kimila waliohudhuria
tamasha la Sabasaba Sanjo ya Busiya ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Machifu Tanzania, Chifu Aron Mikomangwa (Nyamilonda wa Tatu), Mwenyekiti wa
Umoja wa Machifu Usukumani, Chifu Kisendi Joseph Nkingwa (wa Pili) kutoka Himaya
ya Busumabu, Chifu Life Nyanono Barisondole wa Himaya ya Karumo, Chifu George
Sangija wa Himaya ya Sukuma, na Chifu Charles Dotto Balele kutoka Himaya ya
Bujashi.
Hitimisho
Himaya ya Busiya ina jumla ya kata kumi na kwa
takriban miaka kumi na mbili imekuwa ikiandaa matamasha hayo yanayolenga
kuimarisha mila na desturi za Wasukuma.
Tamasha la Sabasaba Sanjo ya Busiya linabakia
kuwa tukio muhimu katika kuendeleza utamaduni na kuhifadhi maadili mema kwa
jamii ya Wasukuma.