Na Mapuli Kitina Misalaba
Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano
ya hadhara wakati wa kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi
wa serikali za mitaa. Lengo ni kusikiliza sera, mikakati, na mipango ya
wagombea, ili kuweza kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Hayo yamesemwa na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Maria Mapunda, wakati
akitoa ujumbe wa Mwenge huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Mapunda
amewakumbusha wananchi umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo
unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024, na kuwasihi wenye sifa
kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali.
Amesisitiza umuhimu wa kuhudhuria mikutano ya hadhara ili kuwajua vyema
wagombea na sera zao, jambo ambalo litawasaidia kuchagua viongozi bora kwa
ajili ya maendeleo ya maeneo yao.
Vilevile, Mapunda amewakumbusha wananchi kuepuka makundi ya kisiasa na
kuzingatia kuchagua mgombea anayefaa bila kushawishiwa na rushwa. Amewataka pia
wananchi kumuunga mkono mgombea atakayechaguliwa kwa maslahi ya wote.
Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Oscar Lupama, ametaja
sifa za mpiga kura na mgombea, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wagombea wote
kuwa raia wa Tanzania.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 ni "Tunza mazingira na Shiriki
uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu."