Mgeni rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akikata utepe katika choo hicho.
Na
Mapuli Kitina Misalaba
Shirika la Companion of Women and Children Empowerment (COWOCE) limefanya hafla maalum leo Ijumaa, Agosti 16, 2024, ya kukabidhi choo cha matundu matatu na chumba maalum kwa ajili ya wasichana katika Shule ya Msingi Mapinduzi B, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga.
Hafla hii imeashiria kukamilika kwa mradi muhimu wa hisani ulioanzishwa na COWOCE, ambao umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mradi huu ulianza rasmi mwezi Machi 2024 baada ya kuundwa kwa kamati maalum ya ujenzi, ikijumuisha wazazi, wanajamii, na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wa karibu na shirika la COWOCE.
Lengo kuu la mradi lilikuwa ni kujenga vyoo vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wa kike, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa miundombinu bora ya afya na usafi shuleni.
Kamati iliyosimamia mradi huu imefanya kazi kwa kipindi cha miezi mitano, na kufanikisha ujenzi wa vyoo hivyo kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni saba.
Mradi huu umepokelewa kwa upendo wa dhati na wanafunzi, walimu, na wazazi, ambao wamefurahia kuona tatizo la muda mrefu la upungufu wa matundu ya vyoo likipata suluhisho.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, amelipongeza shirika la COWOCE kwa juhudi zake kubwa za kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa kike.
Ametoa wito kwa wazazi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha changamoto za wanafunzi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Bi. Agness amewapongeza pia wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha mradi huu, akiwahimiza kuwa umoja huo uendelee katika miradi mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mwalimu James Msimbang’ombe, ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia sana kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa kike, kwani sasa watakuwa na mazingira bora zaidi ya kujifunzia.
Amesisitiza
kuwa ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya kamati, shirika la COWOCE, na
wanajamii umeleta matokeo mazuri, na akaomba juhudi hizi ziendelezwe kwa ajili
ya miradi mingine.
“Kamati ya Hisani katika Jamii iliundwa na wadau wa Maendeleo katika Kata ya Ngokolo kupitia kikao cha wazazi kilichoketi shuleni hapo chini ya usimamizi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali (NGOs) Companion of Women and Children Empowerment (COWOCE”).
"Tarehe 27/02/2024, Shirika la COWOCE lilizindua mradi wa hisani katika jamii katika Shule hii ya Mapinduzi B ambapo wajumbe mbalimbali kutoka serikalini za mtaa na wananchi walihudhuria”.
“Mkurugenzi wa Shirika la COWOCE alitoa mafunzo kuhusu namna mradi wa hisani katika jamii unavyotekelezwa. Baada ya mafunzo hayo, wajumbe walichaguliwa ili kutekeleza mradi wa hisani katika jamii.".
"Kamati iliyoundwa ilikuwa na wajumbe kumi na mbili, akiwemo Mwenyekiti, Katibu, Mratibu pamoja na wajumbe wengine ambao walikamilisha timu nzima ya wajumbe 16 kama inavyoelezwa hapa chini kwa majina na wadhifa wao." amesema Msimbang’ombe
Kamati ya Hisani ilianza kazi rasmi mnamo tarehe 01/03/2024, siku chache tu baada ya kuchaguliwa ambapo zoezi la ukusanyaji wa rasilimali lilianza likiongozwa na Mwenyekiti wa kamati, James Msimbang’ombe.
“Tarehe 01/03/2024 zoezi la ujenzi lilianza, na siku kumi baada ya Kamati kuanza kazi, zoezi la ujenzi lilikamilika tarehe 13/08/2024, miezi mitano baada ya Kamati kuchaguliwa na kuanza kazi."
"Kamati ilitekeleza majukumu yake kwa weredi mkubwa kwa kuzingatia maazimio ya kikao cha wadau ambayo yalitumika kama hadidu rejea katika kutekeleza majukumu ya Kamati."
"Zoezi la ukusanyaji rasilimali na utoaji elimu lilikuwa endelevu tangu siku ya kwanza hadi tarehe ya mwisho likiendelea, kwa sababu mahitaji hayakukusanywa kwa wakati mmoja na kukamilika”.
“Hata hivyo, ujenzi wa choo ulipokamilika bado kulikuwa na mapungufu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu ya maji kwenye vyoo hivyo vya kisasa, jambo ambalo lilibainishwa wakati wa kikao cha tathmini baada ya ujenzi kukamilika."
"Kwa mujibu wa mchoro wa ujenzi na makadirio ya bajeti (BOQ), ujenzi wa choo cha Wasichana Mapinduzi B ulikadiriwa kutumia kiasi cha milioni saba na laki tano (7,500,000). Hata hivyo, ujenzi huu umetumia kiasi cha Tsh 7,806,700. Kamati inaujulisha umma wa wana Shinyanga na Tanzania kwa ujumla kuwa kiasi cha fedha kilichotumika kujenga choo hiki cha kisasa ni Tsh 7,806,700."
"Kamati ya Hisani imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa matundu matatu ya choo
cha wasichana Mapinduzi B pamoja na chumba maalumu cha wasichana kwa ajili ya
kujistiri, hivyo, wasichana watasoma kwa utulivu na mahudhurio yao katika
vipindi darasani yataongezeka, na kuendeleza kiwango cha ufaulu kuwa juu na
ubora wa elimu wanayoipata."
"Mafanikio haya hayakuwa mepesi kwa sababu miradi ya aina hii haijazoeleka katika maeneo yetu na Tanzania hususani Manispaa ya Shinyanga, hata hivyo, umahiri na uvumilivu wa wajumbe wa Kamati umekuwa chanzo kikuu cha mafanikio ya kazi hii ya ujenzi wa choo hiki."
"Kamati inatoa shukrani kwa kuaminiwa kuwa chombo cha kusimamia shughuli hii njema pamoja na kwamba ilikuwa na changamoto, kamati, kwa niaba ya Shirika la COWOCE, inatoa shukrani kwa watu na taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa choo cha wasichana kwenye shule hii umekamilika."
"Kipekee kabisa, japo sio kwa umuhimu, Kamati inatoa shukrani za dhati kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Kamati wakati tulipohitaji ushauri wa kitaalamu, mchango wa mawazo na vifaa kwa ajili ya ujenzi, ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, kupitia wahandisi, wamejitoa kwa kiwango kikubwa kufanikisha ujenzi huu."
"Aidha,
Kamati inashukuru sana Shirika la Companion of Women and Children Empowerment
(COWOCE) wakishirikiana na Shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI) kwa kuja
na mpango ambao umeleta matokeo chanya kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi
Mapinduzi B."
"Tunawashukuru pia walimu na wazazi wa Shule ya Msingi Mapinduzi B kwa ushirikiano wao waliotupatia. Wazazi walichanga michango yao mbalimbali ya vitu na fedha."
"Aidha, Kamati inamshukuru kipekee Jontha Investment kwa mchango wake wa hiari alioutoa katika ujenzi wa choo cha wasichana. Mwisho kabisa, Kamati inawashukuru wote walitoa ushirikiano na kushiriki kwa namna moja ama nyingine kufanikisha ujenzi huu”.
"Kamati ya hisani katika utekelezaji wa mradi huu imebaini kuwa upo uwezekano mkubwa wa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kusaidia jamii yao wao wenyewe, hivyo, tunapendekeza mradi huu utekelezwe mahali pengine katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga."amesema Msimbang’ombe
Mkuu wa Shule ya Msingi Mapinduzi B, Mwalimu Japhet Jasson, pia alitoa shukrani zake kwa shirika la COWOCE kwa kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo shuleni hapo”.
Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa matundu zaidi ya vyoo kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, ambao kwa sasa wanazidi elfu moja ambapo ametoa ombi kwa COWOCE kuendelea na juhudi za kujenga vyoo vingine ili kukidhi mahitaji hayo.
Mratibu wa Ujenzi kutoka shirika la COWOCE, Bi. Grace Moses, amethibitisha kuwa shirika hilo lina mipango ya kuendelea kutatua changamoto ya vyoo shuleni hapo.
Ameeleza kuwa, kwa awamu inayofuata, COWOCE itajikita katika ujenzi wa matundu ya vyoo kwa ajili ya wavulana, hatua ambayo itahakikisha wanafunzi wote wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Meneja wa Miradi wa COWOCE, Nyakabhi Zoma, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, ametoa wito kwa wazazi na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto zilizopo.
Ameeleza
kuwa mafanikio ya mradi huu ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja na kwamba
mshikamano huo unapaswa kuigwa na jamii zingine.
Mwakilishi wa Shirika la Thubutu Africa Initiatives, Bi. Eliaphile Philemoni, naye alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za wadau wanaotekeleza miradi ya hisani kama njia ya kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wetu katika elimu.
Baadhi ya wazazi na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapinduzi B, waliotoa maoni yao wakati wa hafla hiyo, wamelipongeza shirika la COWOCE kwa kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto ya vyoo, ambayo ilikuwa ni kero ya muda mrefu shuleni hapo.
Wameeleza kuwa juhudi za shirika hili zimeleta afueni kubwa kwa wanafunzi wa kike, na kwamba wanatarajia kuona miradi mingine ya aina hii ikiendelea kutekelezwa.
Hafla hii ya kukabidhi mradi wa choo cha wasichana katika Shule ya Msingi Mapinduzi B ni ushuhuda wa jinsi juhudi za pamoja kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali, wazazi, na jamii zinavyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watoto.
Shirika la COWOCE limeahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na shule hilo na wadau wengine katika kuboresha mazingira ya elimu, hasa kwa watoto wa kike ambao wanahitaji zaidi msaada huu.
Mgeni
rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akizungumza
katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi mradi wa hisani kwa jamii leo Ijumaa Agosti 16,2024..
Mgeni
rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akizungumza
katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi mradi wa hisani kwa jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mwalimu James Msimbang’ombe, akisoma taarifa ya ujenzi wa choo cha wasichana shule ya msingi Mapinduzi B.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mwalimu James Msimbang’ombe, akizungumza.
Meneja wa Miradi wa COWOCE, Nyakabhi Zoma, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo
Meneja wa Miradi wa COWOCE, Nyakabhi Zoma, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo
Mratibu wa Ujenzi kutoka shirika la COWOCE, Bi. Grace Moses, akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi mradi wa hisani leo Agosti 16,2024.
Mkuu wa Shule ya Msingi Mapinduzi B, Mwalimu Japhet Jasson, akilishukuru shirika la COWOCE.
Awali baadhi ya wanafunzi wakiimba wimbo maalum wa kulishukuru na kulipongeza shirika la COWOCE.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujenzi, Mwalimu James Msimbang’ombe, akipokea cheti chake cha
pongezi ambacho kimetolewa na shirika la COWOCE.
Mgeni
rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akiendelea
kukabidhi vyeti vya pongezi ambavyo vimetolewa na shirika la COWOCE.
Mgeni
rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akiwa katika
zoezi la kukata utepe.
Mgeni
rasmi, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Bi. Agness Francis, akiwa katika
zoezi la kukata utepe.