SMAUJATA YALAANI TUKIO LA MWANAMKE KUTOBOLEWA MACHO SHINYANGA, YATAKA MTUHUMIWA AKAMATWE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga imelaani vikali tukio la kikatili la kutobolewa Macho kwa mwanamke mmoja, Bi. Esther Matalanga, mkazi wa Mtaa wa Banduka, Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga huku ikiiomba serikali kupitia vyombo vya ulinzi kumtafuta mtuhumiwa na kumkamata ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Bwana Daniel Patrick Kapaya, baada ya kumtembelea na kumpa pole mhanga wa ukatili huo, Bi. Esther, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Kolandoto kwa ajili ya matibabu.

Tukio hilo limetokea tarehe 13 Agosti 2024 katika Mtaa wa Banduka, Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga.

Bwana Kapaya amesema kitendo hicho ni ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu, na ameiomba jamii kuendelea kushirikiana katika kutokomeza matukio ya namna hiyo huku akisisitiza serikali kupitia vyombo vya ulinzi kumtafuta mtuhumiwa na kumkamata ili hatua za kisheria zichukuliwe na iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia mbaya kama hiyo.

“Tupo hapa katika Hospitali ya Kolandoto kumuona mwanamke aliyefanyiwa ukatili wa kutobolewa macho, kwa niaba ya Mwenyekiti wetu wa Taifa, Bwana Sospeter Bulugu, pamoja na Mwenyekiti wetu wa Mkoa, Bi. Nabila Kisendi, tunalaani na kupinga vikali matukio ya namna hii yasijitokeze tena kwa sababu ni ukiukwaji wa haki za binadamu”.

“SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga tumeona bado kuna ukatili unaendelea, ukiwemo unaosababishwa na wivu wa kimapenzi, kujinyonga, na ukatili mwingine wa kuteswa, tunapinga vikali hasa Mkoa wa Shinyanga kwa matukio kama haya, tunawaomba wananchi au jamii kwa ujumla wanapoona matukio kama haya wajitokeze kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa, dawati la jinsia, au watoe taarifa kwa SMAUJATA kwa kupiga simu bure 116 ili kupata msaada,” amesema Kapaya.

“Inaonekana kwamba kwenye maisha ya ndoa, wanandoa wengi wanapata tabu sana kwenye familia, na wengi wanaumia moyoni. Mwisho wa siku yanatokea majanga kama haya, kwa hiyo, tunalaani SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga na tunawaomba wanandoa au kwenye familia wanapokuwa wanapata changamoto kama hizi waziwasilishe mapema ili yasiweze kutokea madhara makubwa kama yaliyompata Ester”.

“Vitendo kama hivi ni ukatili na unyama, na sasa amepewa ulemavu wa kudumu maana alikuwa na uwezo wa kuona, lakini sasa ni changamoto, tunajua hili ni tukio ambalo limeonekana moja kwa moja, lakini kuna matukio ambayo yanatokea kimya kimya. Kwa hiyo, tunatoa tamko kama SMAUJATA na tunaisisitiza jamii kulaani matukio kama haya.”

“Tunaomba viongozi wa dini waendelee kuhubiri amani kwenye nyumba za ibada ili wale ambao hawana hofu ya Mungu wamjue Mwenyezi Mungum kama wangekuwa na hofu ya Mungu, matukio kama haya yasingetokea.”

“Tunaiomba serikali na vyombo vya ulinzi kumtafuta mtuhumiwa ili apatikane na hatua za kisheria zichukuliwe, amejichukulia sheria mkononi, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi, tunaomba mwanaume huyo akamatwe ili iwe fundisho kwa wengine wasirudie matendo kama hayo,” aliongeza Kapaya.

Kwa upande wake, Katibu wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga, Bi. Husna Maige, ameungana na wadau wengine kulaani na kukemea kitendo hicho, akisema kwamba kwa kushirikiana na serikali watahakikisha ukatili unakomeshwa.

“Sisi SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga tunalaani vikali sana tukio la kutobolewa macho kwa sababu Ester amepewa ulemavu wa kudumu, ameshafanyiwa ukatili wa kimwili na pia ameathirika kisaikolojia,huyu ni mama wa watoto wawili, kwa sasa hatoweza tena kufanya majukumu ya kuingiza kipato, na mpaka sasa mtuhumiwa bado hajakamatwa”.

“Tunaiomba serikali kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa kwa sababu ameunda ukatili mkubwa sana, na sisi tutaendelea kushirikiana na serikali kutokomeza ukatili, pia tunawaomba viongozi wa dini waendelee kuhubiri amani makanisani ili kuimarisha imani za waumini wasifanye ukatili na matendo mengine yasiyofaa,” amesema Husna.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dkt. Joseph Wallace Sahani, ameeleza kuwa Bi. Esther anaendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo. "Tulimpokea Bi. Esther akiwa katika hali mbaya. Jicho lake moja lilikuwa limetobolewa kabisa, na lile la pili lilikuwa na majeraha makubwa, kwa sasa anaendelea kupata huduma ya matibabu, na tuna matumaini ya kupona, ingawa jicho moja haliwezi kuona tena," amesema Dkt. Sahani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kumtafuta Paulo Shija, anayesemekana kuwa ndiye aliyefanya ukatili huo dhidi ya mke wake ambapo kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Janeth Magomi ameendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Kwa upande wake, Bi. Esther Matalanga, ambaye ni mhanga wa tukio hili la kikatili, ameishukuru SMAUJATA kwa msaada wao na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya juhudi za haraka kumkamata mume wake, Paulo Shija, ambaye alitoroka baada ya kufanya kitendo hicho.

“Kwa kweli, nawashukuru sana kwa kunitembelea na kunifariji. Mungu awabariki. Nawashukuru sana na muendelee kunitia moyo, nataka serikali wakimkamata huyo mwanaume wampe adhabu kubwa sana,” amesema Bi. Esther kwa hisia kali.

Bi. Ester ametumia nafasi hiyo kueleza chanzo cha tukio hilo, ambapo amesema Paul Shija ni mume wake wa ndoa na walikuwa na mgogorom aliondoka kwenda kwao Kahama, lakini baadaye mume wake akampigia simu akimwambia ameona mwanamke mwingine, hivyo Ester aje achukue vitu vyake ndani na ampe talaka.

“Paul Shija alikuwa mume wangu, tumefunga naye ndoa ya kanisani, lakini tulikuwa na ugomvi mwezi wa tisa mwaka jana, Niliondoka kwenda kwa mama yangu Kahama na nilikuwa nalima huko kijijini, Mwezi wa tatu mwaka huu, alianza kunipigia simu akisema ameshaoa mwanamke mwingine, Nikamwambia haina shida, akaniambia nije nichukue vitu vyangu na anikatie talaka maana tulikuwa tumefunga ndoa, Nikamwambia nitakuja nikipata muda maana nilikuwa na kazi nyumbani”.

“Ameendelea kunipigia simu akiniambia nije nichukue vitu vyangu kwa sababu vinaleta kero ndani, Mnamo Jumapili, alinipigia tena na nikamwambia nitakuja Jumatatu nilipanda gari kutoka Kahama na kufika Shinyanga, nikampigia simu na akaniambia nichukue daladala niende pale anapofanyia kazi Buhangija, nilipofika pale, nikamwambia sasa niongoze nikachukue vitu vyangu, akasema nisubiri mpaka muda wa kutoka kazini, baadaye, saa moja na nusu jioni, mwenzake alipofika, tuliondoka na kuongozana”.

“Ilikuwa ni saa mbili usiku, na aliniambia kuwa usiku umeingia mno na kwamba alikuwa ameshaoa alisema alipokuwa amepanga ni mbali na hapo tulipokuwa, na hakuwa na hela ya daladala, akaniambia nilipie chumba tulale kisha asubuhi tutachukue vitu vyangu, nikakubali, na tulilala, saa kumi ya usiku, aliniamsha na kusema tuende, nilimwambia ni usiku mno, tuvumilie mpaka saa kumi na moja na nusu, alikubali”.

“Ilipofika saa kumi na moja na nusu, tukanyanyuka na kuanza kwenda, tulipita njia ya makaburini huko Musoma Food, tukavuka kamto, ndipo akasema anataka kujisaidia, alirudi nyuma, na mimi nikatangulia, Ghafla alinivuta kanga nilikuwa nimejifunika kanga kwa ajili ya baridi, alipoivua ile kanga, mimi nikakimbia na kuanza kupiga kelele, baadaye alinifuata, akanikandamiza chini huku akinibana miguu na mikono, chini nikiwa namkwaruza mikono yangu usono akanibana mikono akawa ananinyonga badaye mimi nguvu zikaniishia na fahamu zilinitoka yeye akajua kwamba ameniua ndo akaanza kunitoboa macho”ameeleza Ester

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dkt. Joseph Wallace Sahani akielezea hali ya Bi. Ester Matalanga.

Katibu wa SMAUJATA Manispaa ya Shinyanga Bi. Husna Maige akimpa pole Bi. Ester Matalanga.


 

Previous Post Next Post