TAASISI YA WANAWAKE NA SAMIA SHINYANGA YALAANI UKATILI WA KUTOBOLWA MACHO KWA MWANAMKE BI. ESTER MATALANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga imepaza sauti yake vikali dhidi ya tukio la kusikitisha la kutobolewa Macho kwa Bi. Ester Matalanga, mkazi wa Mtaa wa Banduka, Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga.

Taasisi hiyo imesema tukio hilo ni ukatili wa kutisha na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na imetoa wito kwa jamii kupinga vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Tukio hilo, lililotokea mnamo tarehe 13 Agosti 2024, limemwacha Bi. Esther akiwa na majeraha  ambapo kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kolandoto.

Taasisi ya Wanawake na Samia imetembelea Hospitali hiyo kumfariji na kumpa pole Bi. Esther, huku wakilaani kwa nguvu zote kitendo hicho na kutoa wito kwa jamii nzima kuchukua hatua za kukomesha ukatili wa aina hii.

Akizungumza kwa niaba ya Taasisi hiyo, Mwenyekiti Msaidizi wa Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga, Bi. Esther Shida, amewataka Watanzania kuungana kupinga vitendo vya ukatili, akisisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kumsaidia Bi. Esther kifedha ili aweze kupata matibabu stahiki.

"Leo tumemtembelea mwanamke mwenzetu ambaye amefanyiwa ukatili wa kutisha na mume wake, tumekuja kumfariji na tunatoa wito kwa Watanzania wote, hususan wanawake, kupinga na kukataa ukatili wa aina yoyote. Matukio kama haya yanapaswa kushughulikiwa kwa nguvu zote na jamii nzima," amesema Bi. Shida kwa uchungu.

Kwa upande wake, Katibu wa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga, Bi. Tatu Juma Almas, ameiomba Serikali kuhakikisha mtuhumiwa wa tukio hilo anapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wanaume wengine wanaofikiria kufanya vitendo vya kinyama kama hivyo.

"Tuko hapa Hospitalini Kolandoto kumuona na kufahamu hali ya mwanamke mwenzetu. Ninaiomba Serikali ifanye kila jitihada kumkamata mtuhumiwa huyu na kuhakikisha anapata adhabu kali ili iwe fundisho. Wanawake wenzetu tusivumilie manyanyaso kwenye ndoa. Kama mapenzi yameisha, hatuna sababu ya kubaki katika ndoa yenye manyanyaso," amesisitiza Bi. Almas.

Naye katibu wa  Taasisi ya Wanawake na Samia Wilaya ya Shinyanga, Bi. Sada Khamis, ameongeza kuwa bado kuna matukio mengi ya ukatili yanayoendelea katika familia, ambapo amewaomba wazazi na walezi kutofumbia macho vitendo hivyo, hususan kwa watoto ambao ni wahanga wakuu.

Kwa upande wake, Bi. Esther Matalanga, ambaye ni mhanga wa tukio hili la kikatili, ameishukuru Taasisi ya Wanawake na Samia kwa upendo na msaada waliompatia.

Pia, amelitaka Jeshi la Polisi kufanya juhudi za haraka kumkamata mume wake, Paulo Shija, ambaye alitoroka baada ya kufanya kitendo hicho.

“Kwa kweli nawashukuru sana kwa kunifariji mama zangu. Nawashukuru sana na muendelee kuja kunitia moyo, nataka wakimkamata huyo mwanaume wampe adhabu kubwa sana,” amesema Bi. Esther kwa hisia kali.

Misalaba Media imezungumza na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dkt. Joseph Wallace Sahani, ambaye ameeleza kuwa Bi. Esther anaendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo. "Tulimpokea Bi. Esther akiwa katika hali mbaya, jicho lake moja lilikuwa limetobolewa kabisa, na lile la pili lilikuwa na majeraha makubwa, kwa sasa anaendelea kupata huduma ya matibabu, na tuna matumaini ya kupona, ingawa jicho moja haliwezi kuona tena," amesema Dkt. Sahani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kumtafuta Paulo Shija, anayesemekana kuwa ndiye aliyefanya ukatili huo dhidi ya mke wake. Polisi wanaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Taasisi ya Wanawake na Samia imetoa wito kwa jamii nzima ya Shinyanga na Tanzania kwa ujumla, kuhakikisha matukio ya ukatili wa kijinsia yanaripotiwa na kuchukuliwa hatua kali mara moja.

 “Tushirikiane kupaza sauti na kukomesha vitendo vya kinyama vinavyoathiri wanawake na watoto katika jamii yetu, Tunapaza sauti kwa pamoja, tunapambana na ukatili kwa pamoja,” walisema viongozi wa Taasisi hiyo kwa kauli moja.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dkt. Joseph Wallace Sahani akizungumza na Misalaba Media ofisi kwake leo Alhamisi Agosti 15,2024.


 

Previous Post Next Post