Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga imewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la balozi ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, 2024.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,
Husna Mashaka Ally, baada ya taasisi hiyo kupanda miti na kutoa msaada wa taulo
kwa wanafunzi katika shule ya msingi Ibadakuli A na B, shule ya wasichana
Shinyanga Girls, pamoja na kutoa msaada wa sabuni kwenye wodi ya wazazi katika
kituo cha Afya Kambarage mjini Shinyanga.
Husna Mashaka ametumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii
kushiriki kwa amani katika uchaguzi wa serikali za mitaa badaye Mwaka huu,
2024, pamoja na uchaguzi mkuu ujao wa 2025.
Amesema kuwa moja ya malengo ya taasisi hiyo ni
kuwahamasisha wanawake wengine katika masuala ya ujasiriamali, kupinga ukatili,
na kuwafanya akina mama waepukane na mikopo yenye riba kubwa (Kausha Damu),
pamoja na kuzingatia malezi bora kwa watoto ili kuwaepusha na ukatili.
“Nitumie
fursa hii kuwahamasisha akina mama tujitokeze kwa wingi kwenda kujiandikisha
katika daftari la mpiga kura. Vile vile, wanawake muda wa kuchukua fomu ukifika
tusiongope kwenda kuchukua ili kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Mwanamke
yoyote atakayegombea nafasi ya mwenyekiti wa mtaa, ujumbe, nafasi ya mwenyekiti
wa kitongoji, na nafasi zingine, sisi tutamuunga mkono,”
amesema Husna.
Katibu wa Taasisi hiyo, Bi. Tatu Juma Almas, amesema
serikali tayari imeboresha miundombinu ya elimu na amewahimiza wanafunzi kusoma
kwa bidii ili kufikia malengo yao.
“Serikali
hii kupitia Mama yetu Samia amejitahidi kututengenezea mazingira mazuri ili
ninyi muweze kusoma vizuri. Kwa hiyo, niwasihi wanafunzi msome kwa bidii ili
muweze kufikia malengo mliyojiwekea,” amesema Tatu.
Mwenyekiti msaidizi wa Taasisi ya Wanawake na Samia
Shinyanga, Bi. Ester Shida, pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Shinyanga, Bi.
Edith Malidadi, waliwahimiza walimu na wanafunzi kuitunza miti iliyopandwa kama
sehemu ya utunzaji wa mazingira, huku wakiwasisitiza wanafunzi kujiepusha na
makundi mabaya na ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa shule ya Shinyanga Girls, Nurah Wilfred
Kamuntu, aliishukuru na kuipongeza taasisi hiyo kwa msaada wa kupanda miti na
kutoa taulo kwa wanafunzi wa shule hiyo.
“Kitu
hiki ni kikubwa sana na kina thamani kubwa kwenye maisha yetu kama wasichana.
Tunawashukuru sana na Mungu awabariki,” amesema Nurah.
Baadhi ya wanafunzi pia wameishukuru taasisi hiyo
kwa elimu na msaada wa taulo, na kuahidi kusoma kwa bidii ili kufikia malengo
yao.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Husna Mashaka Ally, akizungumza.