Na Mapuli Kitina Misalaba
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imewataka
waandishi wa habari kuhakikisha wanaripoti habari za uchaguzi kwa weledi ili
kuwezesha uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.
Akifungua semina iliyofanyika leo, Agosti 7, 2024,
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amewasihi waandishi wa
habari kutekeleza majukumu yao kwa misingi bora, hasa katika kuelekea uchaguzi
wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka
2025.
Kessy amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari
kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika mchakato wa uchaguzi ambapo
amebainisha kuwa ni jukumu la waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi kuhusu
umuhimu wa kutumia haki na demokrasia kuchagua viongozi bora watakaowaletea
maendeleo.
Amewahimiza waandishi wa habari kuhakikisha
wanaandika habari zilizokamilika na zenye usawa kwa kutoa nafasi kwa pande zote
zinazohusika huku akihimiza umuhimu wa demokrasia, haki za kiraia na kisiasa
kama vile uhuru wa kusema, uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, kuabudu, na
utawala wa kisheria.
“Jukumu la kuzuia rushwa ni lako la langu
tutimize wajibu kwa maana hiyo ninyi waandishi wa habari kama vyombo vya habari
mnawajibu wa kuzuia na kupambana na rushwa katika chaguzi ambazo tunatarajia
mbele yetu uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ambao utafanyika
Mwakani”.
“Waandishi
wa habari tunatarajia kwamba kipindi chote cha uchaguzi tutatimiza maadili yetu
ya uandishi wa habari tusikubali kuingia katika makundi ya kutumika kwahiyo
wito wangu kama ni story zinaandikwa kuhusu uchaguzi basi ziwe ni balanced
story umesikia ya huyo uliza na upande wa pili”amesema
Kessy
“Kwa
mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 8 ibara ndogo ya
kwanza a inasema wananchi ndiyo chimbuko la mamlaka ya utawala wan chi na
kwamba serikali itapata mamlaka kutoka kwao, tunasema nchi yenye demokrasia
kweli husingatia, huhimiza na kuruhusu haki za kuraia na kisiasa kama vile
uhuru wa kusema, uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, kuabudu na kusisitiza
kuhusu utawala wa kisheria”.
“Tunasema
uchaguzi wa viongozi ni muhimu kwa vile unagusa maisha ya wananchi na vitendo
vya rushwa na makosa mengine yanayofanyika wakati wa uchaguzi wa vionozi yanaharibu
uchaguzi na kuwanyima haki baadhi ya wagombea ambao wangesaidia kuleta
maendeleo ya wananchi”.
“Kwahiyo
dhima yetu tunataka wananchi waelewe kuwa baadhi ya wanasiasa hupenda kutumia
rushwa ili kuingia madarakani kwa kuwarubuni wapiga kura ili wawachague kwahiyo
wananchi waelewe kuwa viongozi wa namna hiyo siyo viongozi bora na endapo
watawapa kura zao watarajie kwamba hawatapata maendeleo yaliyokusudiwa”.
“Ikumbukwe
kwamba uchaguzi ni fursa au mchakato ambao watu wenye eneo la uchaguzi wanaitumia
kutafakari mstakabali wa maendeleo yao katika eneo hilo pia ni fursa ya
kuainisha changamoto zote zinazoikabili jamii inayoishi kwenye eneo hilo kwa
kuangalia mahitaji ya eneo lao kwa mfano mahitaji ya Barabara, mahitaji ya
Maji, mahitaji ya Zahanati, mahitaji ya Madarasa na kadhalika”.amesema Kessy
Mwezeshaji wa semina hiyo, Mkuu wa Dawati la Elimu
kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Doo, amesema madhara ya rushwa
katika uchaguzi ni pamoja na jamii kukosa huduma muhimu na maendeleo,
upatikanaji wa viongozi wasio waadilifu, kuongezeka kwa umaskini, na viongozi
wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa kujinufaisha na rasilimali za umma.
Ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea
kushirikiana na kushikamana katika kuzuia na kupambana na rushwa, ambapo
amesema kuwa uchaguzi ni suala muhimu kwa maendeleo ya taifa.