TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI (INEC) YAWAHIMIZA WADAU KUTOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU UMUHIMU WA KUPIGA KURA, WAPIGA KURA WAPYA 209,951 KUANDIKISHWA MKOANI SHINYANGA

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Agosti 9,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wadau wa uchaguzi katika Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupiga kura ili kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwa lengo ni kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.

Rai hiyo imetolewa leo, Ijumaa Agosti 9, 2024, na Makamu Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, wakati wa mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Wadau walioshiriki mkutano huo ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa asasi za kiraia, wahariri wa vyombo vya habari, maafisa habari wa mkoa na halmashauri, pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake, na wazee wa kimila.

Katika hotuba yake, Mhe. Jaji Mbarouk amewahimiza wadau wa uchaguzi kuendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kuboresha taarifa zao vituoni, kwani tume imeweka utaratibu mzuri wa kuwahudumia.

 Ameeleza kuwa tume imeweka utaratibu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito, na akina mama wenye watoto wachanga, ambao watapata fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni.

"Niwaombe wadau wa uchaguzi, tuendelee kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji, na maelekezo ya tume kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari. Uboreshaji huu unawahusu wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura au kuboresha taarifa zao. Hivyo, nawaomba kuhimiza wananchi kupitia majukwaa yenu ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kiimani, na kiuchumi kujitokeza kwa wingi," amesema Mhe. Jaji Mbarouk.

Aidha, amesisitiza kuwa kujiandikisha mara zaidi ya moja ni kosa la kisheria kwa mujibu wa Kifungu Namba 14 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani.

"Mtu yeyote atakayeomba kujiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na atastahili faini isiyopungua shilingi laki moja au kifungo cha kipindi kisichozidi miezi sita au vyote kwa pamoja," ameongeza.

Pia katika mkutano huo yamefanyika majadiliano ya pamoja ambapo wadau mbalimbali wameshiriki kutoa maoni yao huku mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi Mhe. Malozi Omary Mapuri akiahidi tume hiyo kuendelea kuwashirikisha wadau hao katika hatua mbalimbali.

Katika kuhakikisha kuwa zoezi hili linaenda sambamba na matumizi ya teknolojia, INEC imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao utamwezesha mpiga kura aliyeko kwenye daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia simu au kompyuta.

 Hata hivyo, mtumiaji wa huduma hii atatakiwa kufika kituoni ili kukamilisha hatua za kupigwa picha, kuweka saini, na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utawahusu raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi, au watakaotimiza umri huo kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

 Zoezi hilo pia litajumuisha uchukuaji wa alama za vidole, picha, pamoja na saini.

Mkoani Shinyanga, uboreshaji wa daftari utaanza Agosti 21 na kuendelea hadi Agosti 27, 2024. INEC inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 209,951, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 kutoka wapiga kura 995,918 waliopo hivyo, baada ya zoezi hilo, mkoa unatarajiwa kuwa na wapiga kura zaidi ya milioni moja.

Kwa sasa, uboreshaji wa daftari unaendelea katika mikoa ya Kagera na Geita hadi Agosti 11, 2024, ambapo vituo vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inasisitiza kauli mbiu ya "Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora," na imehimiza wadau kuendelea kushiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa zoezi hilo.

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga kwa ajili Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga kwa ajili Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile akizungumza wakati wa mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga leo Agosti 9,2024.Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile akizungumza wakati wa mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga leo Agosti 9,2024.Mkurugenzi wa Mawasiliano jimbo katoliki Shinyanga Padre Anatoly Salawa awali akiongoza sala ya ufunguzi wa mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi Mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Agosti 9,2024. Mkurugenzi wa Mawasiliano jimbo katoliki Shinyanga Padre Anatoly Salawa awali akiongoza sala ya ufunguzi wa mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi Mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Agosti 9,2024.

Waandishi wa habari.




TAZAMA VIDEO

 

Previous Post Next Post