Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea na
uchunguzi kufuatia tukio la kupotea kwa mtoto wa kiume, James Maganga ( Junior),
mwenye umri wa miaka 7, mwanafunzi wa darasa la kwanza na mkazi wa Tinde.
Mtoto huyo
aliripotiwa kupotea tarehe 22 Agosti 2024 majira ya saa mbili na nusu usiku,
baada ya kutumwa na mama yake kwenda kununua maji ya kunywa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baba wa mtoto
huyo, Maganga Saliboko, James alipotea mara baada ya kutoka tena kwenda kununua
maji makubwa, baada ya kurudi awali na chupa ndogo ya maji na kwamba juhudi za
kumtafuta mtoto huyo zilifanyika mara baada ya kutoonekana nyumbani lakini
hazikufanikiwa.
Tarehe 28 Agosti 2024, jeshi la polisi lilipokea
taarifa za kuonekana kwa viungo vya binadamu katika majaruba ya mpunga huko
Tinde ambapo Askari Polisi walifika katika eneo la tukio na kukuta fuvu la
kichwa na taya vinavyoaminika kuwa ni vya binadamu.
Aidha, nguo na kanda mbili zilizokutwa kwenye eneo
hilo zilitambuliwa na baba mzazi kuwa ni za mtoto wake, James.
Hata hivyo, uchunguzi wa kitaalamu bado unaendelea,
ambapo upimaji wa vina saba (DNA) utafanyika ili kubaini kwa uhakika kama
mabaki hayo ni ya mtoto James Maganga (Junior) uchunguzi huu ni muhimu kwa
ajili ya kubaini kilichotokea na kuchukua hatua zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP. Janeth S.
Magomi, ametoa wito kwa wananchi kuwa makini zaidi na kuhakikisha watoto
wanakuwa salama, hasa nyakati za usiku.
Ameonya juu ya tabia ya kuwatuma watoto kufanya
shughuli mbalimbali usiku, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuwaweka katika
hatari kubwa.
SACP. Magom ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa
zinazoweza kusaidia uchunguzi huu kujitokeza na kusaidia ili haki iweze
kupatikana.
Uchunguzi zaidi utaendelea hadi ukweli wote ujulikane.