Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Shinyanga,
Mwl. Paschal Shiluka akizungumza kwenye mahafali ya 12.
Na Elisha Shambiti - Misalaba Media
Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto,
Shinyanga, Mwl. Paschal Shiluka, amewataka wahitimu wa kozi za afya katika chuo
hicho wasiifanye elimu waliyoipata kuwa mali yao bali kuwa mali ya jamii ili
kuweza kuisaidia jamii zao kuondokana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na
afya.
Katika hotuba yake kwenye mahafali ya kumi na mbili (12)
ya chuo hicho yaliyofanyika Ijumaa, Mwl.
Shiluka alisema kuwa wahitimu wanapaswa kutumia elimu waliyoipata kuzigeuza
changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii zao kuwa fursa ambazo zitawaletea
maendeleo binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho,
Dk. Luzila John, amewataka wahitimu hao kwenda kuwa mabalozi wema wa chuo hicho
katika jamii zao kwa kuzingatia maadili mema, kwani elimu na taaluma bila
maadili si kitu chochote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kanisa la African
Inland Church Tanzania (AICT), Mch. Mwl. Josephales Mtebe, amesema kuwa
wahitimu wanapoenda kufanyia kazi taaluma zao wanapaswa kuonyesha upendo na
ukarimu kwa wagonjwa, jambo litakalosaidia wagonjwa kupata nafuu kabla ya
kupatiwa matibabu mengine.
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina
Mzava, ambaye alimuwakilisha mgeni rasmi Naibu Waziri ofisi ya waziri mkuu
kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, katika
mahafali hayo, amesema kuwa wahitimu wanapaswa kujua kuwa serikali haiwezi
kuwaajiri vijana wote wanaohitimu masomo yao na badala yake wajifunze
kujitegemea wenyewe kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii zao kama
vile kutumia fursa za mikopo kwa makundi ya vijana ambayo imekuwa ikitolewa na
serikali.
Mgeni rasmi, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Shinyanga,
Mhe. Christina Mzava akizungumza kwenye mahafali ya 12 katika chuo cha Sayansi
za Afya Kolandoto Agosti 2,2024.
Katibu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church
Tanzania (AICT), Mch. Mwl. Josephales Mtebe, akizungumza kwenye mahafali ya 12
katika chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Agosti 2,2024.