-Asema ni Ujanja Wa wakili Wa Utetezi kupoteza Muda
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kujeruhi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wamekataa kuahirishwa kesi kwa madai kuwa wakili wa utetezi anataka kuchelewesha kesi hiyo kwa kudai kuwa anashida ya kiafya.
Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeomba pande zote mbili katika kesi hiyo kutumia lugha za kuheshimiana ndani ya chumba cha mahakama kwa sababu kuna watu wanajifunza kutoka kwao.
Ombi hilo la kukataa, limewasilishwa leo Julai 6,2024 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo, wakati shahidi Kiran Ratilal akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, Edward Chuwa.
Mwanga amefikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kuomba ahirisho la maswali ya dodoso kwa shahidi Ratilal, kwa madai kuwa hawezi kuendelea kwa sababu ya afya yake na pia kuna dawa za kutumia.
Baada ya Chuwa kudai hayo, Mwanga amedai kuwa hawawezi kukubali ahirisho kwa sababu, wakili huyo alitakiwa kulisema hilo mapema kabla kesi haijaanza kusikilizwa kuwa ikifika muda fulani waahirishe.
"Jamhuri hatuwezi kukubali, wakili alitakiwa kulisema hili mapema anachokifanya ni kutaka kuchelewesha kesi hatuwezi kukubali kuahirisha tunaomba amalize maswali ya dodoso kwa shahidi,"
" Mara ya mwisho alisema anaenda Mahakama Kuu, lakini alivyotoka nje alikuwa anazungumza na vyombo vya habari na pia hakusema anaenda kwenye kesi gani,"alidai Wakili Mwanga
Hata hivyo, Chuwa amedai kuwa siku hiyo hakusema anakwenda Mahakama Kuu, alidai kuna kazi anakwenda kuifanya na pia alikuwa akizungumza na media saa ngapi?
"Naenda kuonana na daktari katika Hospitali Hindul Mandal na siku ya kesi ninaweza kuja na ushahidi hapa mimi nina umri wa miaka 60, nimeomba ahirisho kwa sababu ya ugonjwa,"amedai Wakili Chuwa
Hakimu Lyamuya amesema yeye hayuko kwenye nafasi ya kusema kama Wakili ni mgonjwa au sio mgonjwa kwani hali hiyo ni vile ambavyo mtu mwenyewe anajisikia.
"Kwa sababu umesisitiza kwa umri wako wa miaka 60, mahakama inaahirisha kesi hii kwa nafasi ya mwisho ya kufanya maswali ya dodoso ni haki yako, lakini siku ya kesi itakayotajwa inatakiwa ifike mwisho tusiipeleke hii kesi mbali sana,"amesema Hakimu Lyamuya
Pia, Hakimu Lyamuya aliwataka watumie lugha ya kuheshimiana pale wanapouliza maswali kwa sababu ni watu wengi wanasikiliza, lakini pia kuna wanafunzi washeria ambao wanajifunza kila kitu kutoka kwao.
Hakimu Lyamuya amefikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kumtuhumu Wakili Mwanga kuwa anamsaidia shahidi, baada ya kupinga shahidi wake kuulizwa swali ambalo tayari ameishalijibu.
"Mheshimiwa mimi sijamsaidia shahidi kujibu swali bali nimepinga shahidi kuulizwa swali hilohilo ambalo tayari ameishalijibu,"amedai Mwanga
Kesi imeahirishwa hadi Agosti 15,2024 kwa ajili ya upande wa utetezi kuendelea kumuuliza maswali ya dodoso shahidi.
Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.