WAKULIMA WA TUMBAKU WAPEWA MBINU KUONGEZA UZALISHAJI

Mtaalamu wa Kilimo Michael Zakari alipokuwa akitoa elimu kwa wakulima na wanahabari hawapo picha waliotembelea shamba darasa la Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani hapa (WETCU) mkoani hapa.

Na Lucas Raphael, Tabora.

WAKULIMA wa zao la tumbaku Mkoani Tabora wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea wakati wa msimu mpya wa kilimo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yamebainishwa jana na Mtaalamu wa Kilimo Michael Zakari alipokuwa akitoa elimu kwa wakulima na wanahabari waliotembelea shamba darasa la Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani hapa (WETCU).

Alisema kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kanuni za kilimo bora ni nyenzo muhimu sana kwa wakulima wa zao hilo kwa kuwa itawasaidia kulima kwa tija, kuongeza zaidi na kuongeza kipato chao.

Alibainisha kuwa kwa msimu huu wa kilimo Chama Kikuu Cha Ushirika  wa Wakulima wa Tumbaku (WETCU) kina jumla ya vyama vya msingi (Amcos) 252 ambavyo vinajishughulisha na kilimo cha zao hilo katika maeneo yao.

Zakari alisisitiza kuwa zao hilo kama yalivyo mazao mengine ya kibiashara ni zao la kimkakati linalohitaji uangalizi na matumizi sahihi ya mbolea ili kupata tumbaku yenye ubora mkubwa na kuleta tija katika soko la nje.

Aliongeza kuwa tumbaku bora inavutia wanunuzi wengi zaidi kuja kununua zao hilo hivyo kuwaongezea kipato wakulima na hatimaye kuwawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuchangia pato la taifa.

Mtaalamu huyo wa Kilimo kutoka WETCU alieleza kuwa elimu ya kilimo bora ni uhimu sana kwa kuwa inawapa wakulima uelewa wa matumizi sahihi ya pembejeo na kujua wakati sahihi unaofaa kuanza kulima na namna sahihi ya kutumia mbolea.

Mjumbe wa Bodi ya WETCU Abdallah Iddi alipongeza Chama hicho kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kupitia shamba darasa hivyo akaongeza kuwa elimu hiyo itawasaidia kufikia malengo yao.

Naye Mjumbe wa Bodi hiyo kutoka Wilaya ya Nzega Joyce Mambada alitoa wito kwa wakulima waliopata elimu hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya mbolea.

 

Akiongea kwa niaba ya wakulima wenzake, Msanizi Abeli kutoka kata ya Igalula Wilayani Uyui Mkoani hapa aliwashukuru Viongozi wa WETCU kwa kuja na utaratibu huo wa utoaji elimu kwa wakulima.

 Alibainisha kuwa atatumia elimu hiyo katika msimu huu mpya wa kilimo katika mashamba yake huku ili kupata matokeo chanya na kuahidi kuwa pia atawaelimisha wakulima wenzake manufaa ya kutumia mbolea kwa usahihi ili wapate tumbaku nyingi na iliyo bora.

Aidha mkulima wa tumbaku kutoka Wilaya ya Kaliua Asha Shabani alishukuru Chama Kikuu Cha Ushirika wa Wakulima (WETCU) kwa kuwapa elimu hiyo na kubainisha kuwa sawa watalima kwa tija kubwa zaidi. 

Msanizi Abeli kutoka kata ya Igalula Wilayani Uyui Mkoani hapa mkulma aliwashukuru Viongozi wa WETCU kwa kuja na utaratibu huo wa utoaji elimu kwa wakulima.



 

Previous Post Next Post