Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wametoa wito kwa wahitimu wa kidato cha nne, kidato cha cha sita, cheti na diploma kujiunga na IAA kwa ngazi ya Cheti, diploma, Shahada na Shahada ya Uzamili katika Fani mbalimbali, ili waweze kuandaliwa vema kukabiliana na soko la ajira.
Wito huo umetolewa leo na baadhi ya wanafunzi wa IAA wanaolelewa na Kiotamizi (Incubator) wanaoshiriki Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini katika Viwanja Vya Themi Njiro Jijini Arusha, kuonesha bunifu zao katika teknolojia, biashara na sanaa ambazo zinawasaidia kupata kipato tangu wakiwa chuoni.
Wanafunzi Hao wamesema pamoja na kutoa mafunzo kwa fani zilizopo, IAA kupitia mitaala yake na Kiotamizi inawaandaa wanafunzi kujiajiri na kuajiri wengine kupitia bunifu, vumbuzi na biashara zao kabla na baada ya kuhitimu.
Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili, Shahada ya Sayansi ya Kompyuta, Rolland Matafu anasema pamoja na kusoma Fani hiyo, kupitia incubator Chuo kimemsaidia kuliboresha wazo alilokuwa nalo mpaka kufikia hatua ya kuwa na mfumo huu wa kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kutunza taarifa za mauzo.
"Mimi nimebuni mfumo wa teknolojia ya Mauzo ya Bidhaa (Dream Tech Solution), ambayo itawasaida Wakulima na wajasiriamali kutunza takwimu za mauzo yao, niwaalike watu wote wanahitaji kusoma Chuo waje IAA watapata maarifa na ujuzi kwenye fani zao lakini wataandaliwa kutumia elimu yao kutatua changamoto za jamii na kujipatia kipato na ajira, " alisema Rolland.
Kwa upande wake Meneja wa Kiotamizi cha (IBSUC), Bi. Pamela Chogo amesema anajivunia kuwa na vijana wabunifu, wachapakazi na wadadisi kwani wanaichangamkia fursa waliyopewa na uongozi wa IAA, hivyo wananchi wajitokeze kuona kile wanachokizalisha kupitia sekta ya ujasiriamali na maeneo mengine wakiwa bado masomoni.
IAA inashiriki Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini Viwanja vya Themi Jijini Arusha, Kanda ya Kati Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma na Kanda ya Nyanda za juu Kusini Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Karibu utembelee Banda la IAA ili uweze kupata huduma mbalimbali ikiwemo; Kufanya udahili wa wanafunzi bure, kupata taarifa za kozi mbalimbali, Pamoja na kupata ushauri wa kujiunga na kozi mbalimbali kulingana na ufaulu wa mwanafunzi.