WATANO MBARONI WAKITUHUMIWA WIZI WA INJINI 12 ZA MITUMBWI ZIWA VICTORIA

Bukoba. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limewakamata watu watano kwa tuhuma za wizi wa injini 12 za mitumbwi ndani ya Ziwa Victoria.

Injini hizo za mitumbwi, zimekamatwa katika oparesheni maalumu iliyofanyika Julai 2024, ambayo ilihusisha mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda akizungumza na waandishi wa habari Agosti 12, 2024, amesema watuhumiwa walikamatwa wakiwa na injini hizo zilizopatikana katika maeneo ya Bunda na Musoma mkoani Mara pamoja na Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Mvuvi katika Ziwa Victoria, Muhoja Maige amesema wavuvi wanapata hasara kubwa kutokana na uvamizi wa wezi, hasa kwa vifaa vya uvuvi kama injini ambazo zina bei kubwa.

Maige ameiomba Serikali kuimarisha ulinzi ndani ya ziwa hilo kama ilivyo kwa nchi kavu, ili kulinda rasilimali za uvuvi.

Hata hivyo, imeelezwa kutokana na kuimarika kwa hali ya uvuvi mkoani Kagera, mapato kutokana uvuvi wa samaki yanaongezeka, kwani

mwaka wa fedha 2022/2023, mkoa ulipokea Sh4.5 bilioni na mwaka wa fedha 2023/24 mapato yalipanda hadi kufikia Sh6.16 bilioni.

Ofisa uvuvi mkoani humo, Efrazi Mkama amesema mkoa umefanya ukaguzi wa shughuli za uvuvi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari ya uvuvi haramu.

Mkama amelipongeza Jeshi la Polisi kupambana na wavuvi haramu na ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa za wahalifu hao, ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Previous Post Next Post