Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amesema mchakato wa kuwakamata watuhumiwa wanaodaiwa kumbaka na kumlawiti msichana, anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Mkoa wa Dar es Salaam, unaendelea.
Kauli ya Masauni ni mwitikio wa tukio la video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikionyesha vijana watano wakidaiwa wakimbaka na kumwingilia kinyume na maumbile msichana huyo anayedaiwa kuishi Yombo.
Hata hivyo, kilichoelezwa na waziri huyo kinajibu mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii na hoja za wanaharakati wa haki za binadamu, walioshinikiza Serikali itokea hadharani kukemea na kuchukua hatua.
Miongoni mwa wadau walioshinikiza hatua kwa Serikali ni Meya wa zamani wa Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob kupitia mtandao wake wa X (zamani Twitter), aliyeelezea tukio hilo na kuwaomba viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuchukua hatua.
Jioni ya leo Jumatatu Agosti 5, 2024, Mwananchi imemtafuta Waziri Masauni kujua hasa nini kinaendelea juu ya watuhumiwa hao, akasema vyombo vinavyohusika vinaendelea kulishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.
“Tupo tunalishughulikia. Mchakato unaendelea wa kuwakamata na kuhakikisha tunawapeleka kwenye vyombo vya sheria,” amesema Masauni.
Jana Agosti 4, 2024 Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma kuzungumzia tukio hilo, akieleza wameanza kulifanyia kazi na kulaani, kwa kuwa halikubaliki na ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na haki za binadamu.
"Jeshi limetoa wito kwa wananchi wote waache kuendelea kusambaza video hiyo, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, lakini pia ni kitendo cha kuendelea kudhalilisha utu wa binadamu mwenzetu," amesema Misime na kuongeza:
"Tunatoa wito kwa mwenye taarifa ya kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia kwa haraka waliofanya ukatili huu asisite kutusaidia kwa kutupa taarifa au kumpatia kiongozi yoyote yule wanayemwamini kwamba taarifa ikimfikia watu hao watapatikana haraka iwezekanavyo."
Hali ilivyo mitandaoni
Mapema leo Jumatatu kupitia mtandao huohuo, watu mbalimbali wameanza kuonyesha utambulisho wa vijana hao, wakilitaka jeshi la polisi kuwafikia na kuwakamata, ili sheria ifuate mkondo wake.
Hilda Newton ni miongoni mwa wadau hao ameandika: “Nyie polisi kama mmeshindwa kuwapata hao wabakaji, njoeni hapa kuna details (taarifa) zao na mkifanikiwa kuwakamata tunataka kuona sura zao. Wafikishwe mbele ya sheria na wapewe hukumu sawa na kosa walilotenda, ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.”
Sativa ameandika:”Chaula alipochoma picha ya Rais haikupita hata saa 10 kabla hajakamatwa. Hebu tupaze sauti hawa wabakaji wapatikane bila kujali vyeo vyao na aliyewakodi atiwe nguvuni.”
Katika mwendelezo huo wa kushinikiza sheria ichukue mkondo wake, Wakili Peter Madeleka amesema atalazimika kuingilia kati suala hilo kama Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hatachukua hatua ndani ya saa 24.
“Nataka nimwambie DPP ikiwa ndani ya saa 24 kuanzia sasa atashindwa kuwapeleka mahakamani hawa mashetani kwa kisingizio chochote. Mimi Peter Madeleka nitafanya wajibu huo kwa fedha zangu. Hatuwezi kuwa na Taifa la kulinda wahalifu.
“Nitakwenda mahakamani ili kuiomba Mahakama iwalazimishe polisi na taasisi nyingine zitimize wajibu wao haki ya mwanamke aliyebakwa na kulawitiwa ipatikane haraka iwezekanavyo” ameandika Madeleka.
Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inaonyesha namna msichana huyo akifanyiwa ukatili huo, pamoja na mambo mengine ilisikika sauti vijana hao wakidai wametumwa na afande kulitekeleza hilo kwa kile kinachodaiwa msichana huyo alitembea na mume wa mtu.
Walichokisema LHRC, TLS
Mbali na watumiaji wa mitandao, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani kitendo hicho cha kikatili na unyanyasaji wa kijinsia na kumuomba Rais Samia kutoka hadharani kuonyesha kuchukizwa na tukio dhidi ya msichana huyo anayedaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema kituo hicho kama sehemu ya jamii imehuzunishwa na ukatili huo na kutaka wahusika wote watano na aliyewatuma kulingana na maelezo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Henga amesema matukio kama hayo yakifumbiwa macho yatazidi kujitokeza zaidi katika jamii.
"Vyombo vyote vya ulinzi na usalama viungane katika kuwatambua na kuwakama wahusika na wachukulie hatua," amesema.
Pia, ametoa wito kwa jamii kupaza sauti na kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha haki inapatikana na hatua kali zinachukuliwa dhidi ya waliohusika. Amesema tukio hilo pia ni kosa la jinai la ubakaji wa kundi (gang rape) kwa mujibu wa sheria ya kanuni za adhabu (Penal Code Cap 16) Kifungu kwa 131A adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Mbali na ubakaji huo pia, kuna makosa mengine ya jinai kama kumwingilia mtu kinyume cha maumbile (unnatural offence) na kusambaza picha chafu mtandaoni ambalo ni kosa la kimtandao," amesema.
Tukio hilo pia limemuibua rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi aliyelitaka Jeshi la Polisi lichukue hatua stahiki za kisheria na kuhakikisha wahalifu wote waliotenda kitendo hicho na waliowezesha wakamatwe na kufikishwa mahakamani, ili haki itendeke.
Kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma leo, Mwabukusi amesema tukio hilo si tu kinyume na sheria za nchi, pia ni kinyume na maadili na utamaduni wa Watanzania.
Aidha, amesema TLS inapinga vitendo vyote vya kikatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na iko tayari kushirikiana na vyombo vyote vya usalama na haki jinai katika kuhakikisha wahalifu hao wanafikishwa katika mamlaka sahihi za haki, ili kujibu mashtaka yao.
“TLS pia kupitia kifungu cha 4 (e) cha Sheria iliyounda TLS (Tanganyika Law Society Act, Cap. 307 R.E. 2002) inaendelea kufuatilia mwenendo wa suala hili kwa ukaribu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na vinavyosimamia haki jinai, ili kuhakikisha hatua stahiki kwa waliohusika zinachukuliwa kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.
“Kila binadamu anastahili heshima, haki na usawa katika jamii yetu. TLS inatoa wito kwa jamii kusimama pamoja kupinga udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia wa aina yoyote ile, ikiwemo kuacha mara moja kusambaza video zinazohusu tukio hili ili kulinda haki ya mhanga,” amesema Mwabukusi.
Chanzo - Mwananchi