Na Mwandishi Wetu- Misalaba Media
Zaidi ya shilingi milioni 600 zinatarajiwa kutumika kujenga shule mpya ya sekondari katika kata ya Kisumwa, wilayani Rorya. Mradi huu unalenga kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu, hali ambayo imekuwa ikipunguza kiwango cha ufaulu wilayani humo.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara, Mbunge wa jimbo la Rorya, Mhe. Jafari Chege, aliwatoa hofu wakazi wa kata ya Kisumwa kuhusu changamoto ya ukosefu wa shule iliyo karibu. Aliwahimiza wawe na subira kwani shule mpya inayotarajiwa kujengwa itasaidia kuondoa changamoto hiyo na kuwapa wanafunzi fursa ya kupata elimu kwa urahisi.
Katika mkutano huo, Mhe. Chege alipata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya simu na Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Ndg. Sospeter M. Mtwale, na kumweleza changamoto zinazowakumba wakazi wa kata ya Kisumwa. Mhe. Chege alimuomba Naibu Katibu Mkuu kuhakikisha shule hiyo inajengwa haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake, Ndg. Mtwale aliahidi kwamba ifikapo Januari 2025, shule hiyo itakuwa tayari imekamilika na itaanza kupokea wanafunzi kwa ajili ya kupata elimu bora.
TAZAMA VIDEO