Bara la Afrika limejaaliwa kuwa na mila na desturi nyingi ambazo zinafahamika na zingine ambazo hazifahamiki kwa ulimwengu mzima, nyingi kati ya mila hizo ambazo hazifahamiki zinapatikana katika sehemu za ndani sana na zisizofikika kirahisi.
Zifuatazo ni mila na desturi tano ambazo si za kawaida zinazofanywa na baadhi ya makabila barani Afrika.
Kuiba mke kwenye ngoma za usiku
Mila hii inatekelezwa na kabila ndogo la Wodaabe linalopatikana kati ya kaskazini mwa Nigeria, kusini mwa nchi ya Cameroon, magharibi mwa Afrika ya Kati na kusini mwa nchi ya Chad ambapo wakati wa sherehe za kimila, jamii hiyo hujumuika katika ngoma za usiku. Na katika usiku huo wanaume wanaruhusiwa kuiba mwanamke yoyote na kwenda kustarehe naye hadi asubuhi bila kujali mwanamke huyo ameolewa ama la!, isipokuwa mwanamke mwenyewe akikataa .
Kupima urijali wa bwana harusi
Tamaduni hii inapatikana nchini Uganda kwenye kabila la Banyankole, ambapo shangazi wa bibi harusi mtarajiwa hushiriki tendo la ndoa na bwana harusi ili kupima kama mwanaume huyo ni rijali kabla ya harusi haijafungwa. Makabila mengine nchini humo hulazimika kusikiliza dirishani wakati bwana na bibi harusi wakishiriki tendo la ndoa.
Kuruka kundi la ng’ombe
Nchini Ethiopia, kijana kabla hajafuzu kuingia katika hatua hiyo hupimwa kwa kupewa jaribio la kukimbia na kuwaruka kundi la ng’ombe ambao wamepangwa katika mstari akiwa uchi, tukio linalojulikana kwa jina la ‘Hamar’ ambapo baada ya kumaliza, marafiki wa kike wa kijana huyo humponya majeraha yake kwa mafuta kisha hucheza ngoma na kufurahi pamoja.
Kuvumilia kipigo ili kupata mke na heshima
Kwenye jamii ya fulani nchini Benin, wanaume ambao wanahitaji kuanzisha familia hawana budi kuvumilia kipigo kutoka kwa wazee wa jamii hiyo endapo upande wa mwanamke utachagua utaratibu huo unaojulikana kama ‘ Sharo’ . Endapo mwanaume atashindwa kuvumilia kipigo hicho basi taratibu za harusi hiyo zitavunjwa na inakuwa ni aibu kubwa kwake na familia yake.
Sherehe za mazishi
Katika taratibu za mazishi za kabila la Chewa nchini Malawi, hufanya utaratibu wa siri unaojulikana kama ‘Nyau’ ambapo hufunika nyuso zao kwa maski wakati wa mazishi. Huanza kwa kuuosha mwili wa marehemu kwa kuumwagia maji kisha hayo maji ambayo yanaoshewa maiti hutumika kwa kutengenezea chakula ambacho huliwa na watu wote wanaohudhuria katika mazishi hayo.