Ticker

6/recent/ticker-posts

ASASI ZA KIRAIA KUACHA ALAMA KATIKA JAMII

 
Na Bora Mustafa, Misalaba Media, Arusha.
         
Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services 
Facilities (LSF )Lulu Mwanakilala ameshauri Mashirika kujifunza kuacha alama za maendeleo katika jamii baada ya muda wa utekelezaji wa mradi kuisha. 

Akizungumza katika siku ya nne ya wiki ya CSO Jijini Arusha, amesisitiza  taasisi kuwafundisha wananchi kupenda na kuheshimu miradi katika maeneo yao, hatua itakayowafanya kujisimamia na kubuni miradi mingine ya kuwaongezea kipato. 

"Mfano mzuri ni ule mradi wa Legal Services Facility tunaotekeleza Wilayani Longido, Wale Wamama wa Kimasai wanajiongeza kubuni miradi mingine midogomidogo ndani ya mradi mkubwa ili kuongeza kipato chao, hii ina maana hata mradi ukiisha wataendeleza jitihada za kujikwamua na umasikini" ameendelea kusema, 

"Ikumbukwe kwamba, kufanya kazi na jamii ni wito, ukitanguliza maslahi huwezi kufanya kazi na jamii, nakumbuka sisi tukianza harakati za kufanya kazi na jamii miaka 20 iliyopita, hatukuwa na pesa wala ofisi tulikuwa chuo hivyo tulitumia pesa tulizopewa kama mkopo (bumu) kuwasaidia waathirika wa Ukimwi kipindi hicho, kuwapa elimu kuhusu lishe na masuala mengine, ndipo safari yetu ilipoanzia" ameeleza Mwanakilala. 

Rais wa AZAKI  Dkt.Stigmata Tenga ameyahimiza mashirika na taasisi kuacha kubweteka bali kufikiri kuanzisha mfuko wa AZAKI utakaosaidia kuendeleza utekelezaji miradi, hali itakayoleta ushawishi kwa taasisi nyingine kubwa kuongeza nguvu katika hili. 

"Hatuwezi kupinga kwamba tunategemea pesa za miradi kutoka mashirika ya nje ili kujiendesha,  inafikia wakati ukienda nchi za nje unaogopa kutaja unatokea kwenye taasisi fulani, sababu tunasifika kwa kutegemea misaada, tujitafakari ni lini tutaweza kusimama bila misaada kutoka nje" amehoji Dkt. Tenga. 

Aidha ,Justice Rutenge ambae ni Mkurugenzi Mtendaji wa (AZAKI) amesema Asasi ziache kuwatumia wananchi kujinufaisha na kuwageuza kuwa vyanzo vya kujilimbikizia mali. 

"Tunapofanya kazi na jamii ni vema kuwaelimisha na kuwajengea uwezo, kujua haki zao za msingi, mfano mwanamke akifanyiwa vitendo vya ukatili aende wapi na kwa wakati gani,  naamini jamii wakielimishwa mabadiliko yatakuwa makubwa na kuleta matokeo chanya" amefafanua Rutenge. 
       
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Equality For Growth Jane Magigita ameeleza kuwa, asasi za kiraia zinahitaji uhuru Ili ziweze kuamua nini kitekelezwe na kwa mahali gani, badala ya wahisani kukupangia maeneo gani yazingatiwe katika kutekeleza miradi.

"Tunataka uhuru katika utekelezaji na tunafanya mambo makubwa, mfano Mama wa Sokoni amebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa, amejitambua na anaweza kuwa yeyote anayetaka kuwa" amesema Magigita.



Post a Comment

0 Comments