ASKOFU BUGOTA AHIMIZA JITIHADA ZA KIROHO NA MALEZI YA FAMILIA, MHE. LUCY MAYENGA APONGEZA AICT KWA MAFUNDISHO YENYE TIJA KWA JAMII

 

Askofu Msaidizi wa Kanisa la AICT Tanzania, ambaye pia ni Askofu wa Makanisa ya AICT Dayosisi ya Shinyanga, Zakayo Bugota akitoa salamu zake kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Askofu Msaidizi wa Kanisa la AICT Tanzania, ambaye pia ni Askofu wa Makanisa ya AICT Dayosisi ya Shinyanga, Zakayo Bugota, amewasihi wanawake wa Dayosisi ya Shinyanga na waumini kwa ujumla kuendelea kumtumainia Mungu ili wapate nguvu za ushindi maishani.

Akizungumza katika mkutano wa kiroho wa wanawake wa AICT uliofanyika leo katika viwanja vya Kanisa la AICT Kambarage, mjini Shinyanga, Askofu Bugota amewataka wanawake kuimarisha jitihada zao katika malezi ya familia kupitia mafundisho ya neno la Mungu.

Askofu Bugota amesisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki maombi, akiwasihi waombee familia zao na taifa kwa ujumla, hasa kuelekea chaguzi za serikali za mitaa mwezi Novemba na Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Amesema ni jukumu la wanawake kuwafundisha watoto wao neno la Mungu kupitia vipindi vya Sunday school na kambi mbalimbali, na pia kuwasaidia vijana kuacha kujiingiza katika mitindo isiyompendeza Mungu.

“Ongezeni jitihana katika kushiriki maombi mkijiombea kwanza ninyi wenyewe na kuombea familia zaidi, muongeze bidii zaidi katika kizazi hiki cha sasa hivi kusaidia maisha ya vijana wakiwemo mabinti kuendelea kumtegemea zaidi Mungu badala ya kujiingiza katika mitindo ya kimbingu kwahiyo ni jukumu kubwa sana na kwenu wanawake ambao wengi ni wazazi kutumia neno la Mungu kusaidia kizazi tulichonacho ambacho kinakabiliwa na hatari nyingi zaidi”.

“Kila mwanamke mcha Mungu hawezi kusahau kuliombea taifa hili na ulimwengu wote kwa ujumla mwezi wa Novemba na Mwakani tutakuwa na chaguzi mbalimbali katika nchi hii ikiwemo serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwahiyo nawasihi sana tuendelee kuliombea zoezi hili lifanikiwe ili kupata viongozi bora watakaolisaidia taifa hili”.amesema Askofu Bugota

Kwa upande wake mgeni rasmi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, amewapongeza wanawake wa AICT kwa mafundisho yao yenye msaada mkubwa katika jamii.

Mhe. Mayenga ameongeza kuwa changamoto nyingi zinazokumba jamii, zikiwemo suala la afya ya akili, zinahitaji elimu na mafundisho mazuri kama hayo ili kuwasaidia wanawake kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

“Dunia hii kwa sasa hivi kwa kweli tusipokuwa waangalifu sisi kama wanawake tukarudi nyuma kujiuliza ni nini dhumuni la Mungu kutuleta hapa Duniani kuna baadhi ya vitu havitaweza kwenda kwahiyo nimefarijika sana na mafundisho yote ambayo yamefundishwa na idara hii ya wanawake kwa kweli mnatoa mafundisho mazuri sana”.amesema Lucy Mayenga

“Zipo changamoto nyingi sana ambazo zinaendelea kwenye jamii yetu lakini baadhi yake zinasababishwa na watu kutokuelewa lakini watu wengine ambao wamekumbwa na madhira mbalimbali katika Dunia yetu kutokana na changamoto mbalimbali za maisha wamekata tama na hao wapo wengi mpaka tumepata msamiati wa suala la afya ya akili”.

“Wakina mama sisi huwa ni wapambanaji sana na wavumilifu kwa kiasi kikubwa lakini wakati mwingine watu wanakuwa wanashindwa kuvumilia wanaendelea kwahiyo elimu kama hii itasaidia sana kuwatoa akina mama kuacha kufanya mambo ya ajabu na kufanya mambo ambayo Mungu anapendezwa nayo”.amesema Lucy Mayenga

Kilele cha mkutano wa kiroho wa wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga kimefanyika leo Jumapili Septemba 8,2024 katika viwanja vya kanisa la AICT Kambarage mjini Shinyanga ambapo mhubiri katika mkutano huo ni Mwinjilisti Esther Shija kutoka jimbo la Kahama.

Kaimu Mratibu wa Idara ya Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Bi. Eliaremisa Shilinde, akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa dayosisi hiyo, ameelezea jitihada zinazofanywa na idara hiyo katika kuwahudumia wanawake na jamii kwa ujumla.

Risala hiyo imeweka bayana malengo na changamoto zinazowakabili wanawake wa AICT, huku ikijikita zaidi katika kuleta mabadiliko kupitia mafundisho ya kiroho na kijamii.

Bi. Shilinde amesisitiza umuhimu wa kuwainua wanawake kupitia elimu ya Neno la Mungu na ujasiriamali kupitia semina, makongamano, na mikutano ya uinjilisti, idara ya wanawake inalenga kuwapatia wanawake maarifa ya kutosha, si tu kwa maisha ya kiroho, bali pia kwa kuboresha hali zao za kiuchumi.

Idara ya wanawake ya AICT imeweka wazi malengo yake yanayojikita katika kuboresha maisha ya wanawake, si tu kwa kuimarisha imani yao, bali pia kwa kutoa elimu ya ujasiriamali hii inalenga kuwasaidia wanawake kuongeza kipato na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Pia, idara inatoa elimu juu ya masuala mtambuka kama utunzaji wa mazingira na tahadhari za kiafya, ikiwa ni pamoja na kupanda miti na kuhamasisha jamii juu ya magonjwa ya mlipuko.

Idara hii pia imeweka mkazo katika kuwasaidia mabinti kupitia semina za kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujilinda, na kufikia malengo yao katika risala yake, Bi. Shilinde ameeleza kuwa idara inafanya kazi za utetezi kwa wale wanaokabiliwa na changamoto kama uonevu na ukatili wa kijinsia.

Pamoja na mafanikio, idara hiyo pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ongezeko la wajane, na mmomonyoko wa maadili ambapo Bi. Shilinde ameonyesha masikitiko kuhusu ongezeko la vitendo vya utekaji na ulawiti wa watoto, akisema kuwa wanawake wa AICT wameshikamana katika kupinga vitendo hivi na kuendelea kutoa wito wa haki kuchukuliwa dhidi ya wahalifu.

Kuhusu ongezeko la wajane, Bi. Shilinde ameeleza kuwa idadi ya wajane inaongezeka kwa kasi, huku wengi wao wakikabiliwa na changamoto za kimaisha ambapo idara hiyo pia imekuwa ikiendesha makongamano maalum ya kuwasaidia wajane, likiwemo kongamano la wajane lililofanyika Musoma, ambapo wajane 120 kutoka Dayosisi ya Shinyanga walihudhuria.

Kwa upande wa maadili, Bi. Shilinde ameelezea dhamira ya kanisa la AICT katika kupinga mmomonyoko wa maadili, hususan miongoni mwa vijana ambapo amesema idara ya wanawake imekuwa ikijitahidi kutoa elimu ya maadili kwa waumini na jamii kwa ujumla, huku ikipinga vikali tabia zisizo za staha kama ushoga na mavazi yasiyofaa.

Aidha, Bi. Shilinde ametoa wito kwa serikali kuendelea kuwasaidia wanawake kupata mitaji ili kujikwamua kiuchumi, hasa wale waliotelekezwa na waume zao katika risala hiyo, ameweka wazi kuwa idara ya wanawake ya AICT imeanzisha mradi wa ujenzi wa hostel kwa lengo la kukuza uchumi wa idara hiyo na kuwasaidia wanawake kiuchumi na kiroho.

Akihitimisha risala yake, Bi. Shilinde amesisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambapo amesema kuwa kanisa la AICT limejiandaa kuchagua viongozi wenye maadili na wanaoongozwa na hofu ya Mungu. Aliwahimiza wanawake wa AICT kushiriki kikamilifu ili kujenga jamii yenye maadili na mshikamano.

Askofu Msaidizi wa Kanisa la AICT Tanzania, ambaye pia ni Askofu wa Makanisa ya AICT Dayosisi ya Shinyanga, Zakayo Bugota akitoa salamu zake kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Mgeni rasmi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, akizungumza kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Mgeni rasmi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, akizungumza kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Mgeni rasmi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, akizungumza kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Kaimu Mratibu wa Idara ya Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Bi. Eliaremisa Shilinde, akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa dayosisi ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa idara ya Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Bi. Suzy Kifutumo akitoa shukurani kwa viongozi, wadau na waumini ambao wameshiriki mkutano huo.

Bernadetha Clement Mathayo mke wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko, akitoa salamu zake kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.

Bernadetha Clement Mathayo mke wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko, akitoa salamu zake kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga Septemba 8,2024.








Mwinjilisti Esther Shija akihubiri kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga katika viwanja vya Kanisa la AICT Kambarage Septemba 8,2024.

Mwinjilisti Esther Shija akihubiri kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga katika viwanja vya Kanisa la AICT Kambarage Septemba 8,2024.

Mwinjilisti Esther Shija akihubiri kwenye mkutano wa kiroho wa Wanawake wa AICT Dayosisi ya Shinyanga katika viwanja vya Kanisa la AICT Kambarage Septemba 8,2024.

 

Previous Post Next Post