Na Mapuli Kitina Misalaba
Kastory Kashinje Shija, Baba mzazi wa marehemu
Charles Kashinje, ameliomba Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kufanya uchunguzi
wa kina ili kubaini waliohusika na mauaji ya mtoto wake.
Charles Kastory Kashinje, mwenye
umri wa miaka 24 na mkazi wa kijiji cha Idodoma, kata ya Samuye, Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga, alikutwa akiwa ameuawa kwa kukatwa sehemu mbalimbali za
mwili wake kando ya barabara usiku wa kuamkia
Jumatatu, Septemba 9, 2024.
Misalaba Media imezungumza na Baba wa marehemu,
Kastory Kashinje Shija, ambaye ameliomba Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga
kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na mauaji hayo na kwamba amesema
marehemu alikuwa mtoto wake wa mwisho kati ya watoto kumi na ameacha watoto
wawili wa kike.
“Mimi
nalipongeza jeshi la polisi walikuja tukashirikiana nao, mimi nawategemea
wafanye mbinu zote hao watu waliofanya hivo wajulikane, wapatikane hilo tu nataka
wajulikane maana sina lakufanya kabisa mtoto wangu amechinjwa kama kuku tena
likuwa namtegemea alikuwa mtu mzuri sana hao watu labda alikuwa anawadai inawezekana
walikuwa wenyeji wake ndiyo maana wakafanya hivo wakaona tusimbakize tumchinje
kabisa yaani familia yangu alikuwa anahudumia kila kitu nilikuwa namtegemea
sana, mimi ninawatoto kumi (10) huyo Charles alikuwa ni mtoto wangu wa mwisho
ameacha watoto wawili wote wa kike”.amesema Baba mzazi
Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga,
ACP Kennedy Mgani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa
uchunguzi bado unaendelea.
"Ni kweli tukio lilitokea, lakini mpaka
sasa hakuna mtu aliyekamatwa maana ufuatiliaji bado unaendelea, uchunguzi
unaendelea bado hatuna update zaidi watiliwa mashaka na wengine kwahiyo bado
uchunguzi unaendelea" amesema
ACP Mgani.
Misalaba Media itaendelea kufuatilia tukio hilo na kutoa taarifa zaidi.