Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. BITEKO ASISITIZA MAADILI, WELEDI NA UWAJIBIKAJI KATIKA UNUNUZI WA UMMA

Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Doto Mashaka Biteko amezitaka Taasisi na idara mbalimbali kufuata kanuni na sheria katika manunuzi ya umma .
Aidha Biteko amesema kuwa ,ni lazima fedha zinazotumika katika manunuzi ya umma zikafuata sheria ili kuongeza tija katika miradi mbalimbali ya maendeleo. 
Dkt. Biteko ameyasema hayo  leo Septemba 09, 2024 kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC Jijini Arusha, alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Kongamano la 16 la ununuzi wa umma la Afrika ya Mashariki na uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki wa ununuzi wa umma (NEST) .
Dkt. Biteko amesema kuwa,sekta  hiyo ni muhimu sana  na mambo hayo yasipotiliwa  mkazo wananchi hawawezi kupata huduma bora hivyo ni lazima  wahakikishe wanazingatia maadili  ili huduma iweze kuwepo .
“Kama hatuna idara au taasisi imara za manunuzi miradi iliyopo haiwezi kutekelezeka ipasavyo  kwani manunuzi mengi  yasiposimamiwa vizuri vitendo vya rushwa vitaendelea kuchukua nafasi kubwa.”amesema  Biteko.
Aidha amewataka   wanataaluma hao kulinda taaluma zao  ikiwa ni pamoja na kukumbushana wajibu wao huku akiwataka kuonea wivu taaluma yao na kukemea tabia ambazo hazifai.
“Nawaomba sana muwe wakali  kuwakemea  wanataaluma wote wanaowarudisha nyuma kwa vitendo visivyofaa ninyi wote mumkasirikie na kumnunia kwasababu baadae lawama zitakuja kwenye taaluma yenu.”amesema Dkt.Biteko.
” Naomba Waziri wa Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Kupitia majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji na bila maadili wananchi hawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo ya fedha na hatimaye umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza mwaka 2001 kwa kutungwa kwa Sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma. Baada ya changamoto kadhaa, zilipelekea mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). 
“Serikali kupitia PPRA kama chombo cha Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ililenga kufanya mageuzi na kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, kuhakikisha thamani ya fedha, uwazi, na uwajibikaji, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi na kujenga uwezo katika ununuzi na ugavi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amebainisha Dkt. Biteko.
Ametaja maboresho yaliyofanywa na Serikali kuwa ni kuboresha mfumo wa kisheria na kuweka miundo ya utawala, uboreshaji wa mifumo ya kidijitali, kuajiri na kuwajengea uwezo wafanyakazi, kuboresha upatikanaji wa zabuni kwa Watanzania ambapo ametolea mfano kuwa wazawa wakijengewa uwezo wanaweza kufanyakazi vizuri hata nje ya nchi, pamoja na kuimarisha vita dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumzia mfumo wa NeST, Dkt. Biteko amefurahishwa na mfumo huo kujengwa na vijana wa Kitanzania ambao nchi nchi nyingi za Afrika Mashariki zimeanza kuutamani mfumo  huo ambao umekuwa na faida za kupunguza gharama za kufanya ununuzi kwa wazabuni wa Serikali, kuondokana na matumizi ya karatasi, kuongezeka kwa kasi ya ununuzi pamoja na kupunguza makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad H. Chande ameipongeza Serikali kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta tofauti tofauti nchini ikiwemo sekta ya ununuzi wa umma ambao umeonesha kuwa na tija katika sekta hiyo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El Maamry Mwamba amesema kuwa Jukwaa hilo linalenga kuwakutanisha wadau kuzungumzia masuala ya ununuzi wa umma kwa  manufaa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa mwaka 2024 linafanyika nchini Tanzania na kuandaliwa na Wizara ya Fedha. 
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na kuleta tija ya kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha inayoonekana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma (PPRA),  Dennis Simba amesema kuwa majukwaa hayo hukutana kupitia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo huwa na majadiliano na maazimio na katika Jukwaa la 16 washiriki watapata fursa ya kuangalia utekelezaji wa maazimio ya jukwaa la 15.
“Kupitia mada mbambali washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika ununuzi wa umma na kusaidia nchi wananchama kuboresha ununuzi wa umma na kushughulikia changamoto zilizopo katika ununuzi wa umma.” Amesema  Simba.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba ametaja moja ya jukumu la taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa umma na inatambua kuwa ununuzi wa umma nchini ni eneo linalohitaji kusimamiwa vizuri ili kuleta matokeo tarajiwa.
Mhandisi Ndomba ameongeza kuwa sambamba na kusimamia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Uendeshaji Shehena na Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG), eGA inasimamia pia Mfumo wa ununuzi wa NeST.
Aidha Jukwaa hilo la 16 limeongozwa na kauli mbiu inayosema “Utumiaji wa Mifumo ya Kielektroniki kwa Ununuzi wa Umma Endelevu. 

Post a Comment

0 Comments