GAKI INVESTMENT YAONYESHA MAFANIKIO, WAZIRI BASHE APONGEZA JITIHADA ZA KUIMARISHA UZALISHAJI WA PAMBA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohammed Bashe, leo Septemba 12, 2024 amefanya ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga ambapo amepata fursa ya kutembelea kiwanda cha Gaki Investment kinachojihusisha na uchakataji wa zao la pamba.

Ziara hiyo inalenga kuangazia umuhimu wa kuongeza thamani ya pamba kwa wakulima wa mkoa wa Shinyanga  na taifa kwa ujumla.

Akiwa kiwandani hapo, Waziri Bashe amepongeza juhudi zinazofanywa na Gaki Investment katika kuboresha uchumi wa wakulima kupitia uchakataji wa pamba ambapo amesisitiza kuwa uwekezaji kama huo unachangia kuinua kipato cha wakulima na kusaidia kuongeza ajira kwa wakazi wa Shinyanga.

"Ni muhimu sana kuona sekta binafsi ikishiriki kikamilifu katika kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu, ushirikiano huu ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo," amesema Waziri Bashe.

Aidha Waziri Bashe ametumia ziara hiyo kuhimiza wakulima na wanunuzi wa pamba kujikita zaidi kwenye uzalishaji wenye tija badala ya kuingiza siasa katika kilimo.

Amesisitiza kwamba programu za ugani zinazotekelezwa na wanunuzi kama Gaki zimeonyesha mafanikio makubwa, na hivyo ni muhimu kwa serikali na wadau waendelee kushirikiana ili kufikia malengo ya kuimarisha sekta ya kilimo.

"Tupo mkoani Shinyanga na tunaendelea na ziara leo tumekuja kutembelea kiwanda cha GAKI Investment, Gaki ni mmoja wa wanunuzi wa pamba, na pia ni mmoja wa wanunuzi waliokubali kushiriki kwenye programu ya ugani tuliyoianza msimu uliopita wa kilimo, yeye mwenyewe amesema kuwa uzalishaji uliotokea katika kata za Mbutu, Kishapu, na Meatu umekifanya kiwanda chake kufanya kazi kubwa, na mahitaji yake yote amenunua kutoka kwenye kata alizowekeza”.

“Jambo moja ambalo nataka kusema ni kwamba, katika nchi yetu, zao la pamba limegeuka kuwa suala la siasa badala ya kuwa zao la kiuchumi. Ukiangalia ukanda huu wote, wakulima wanaishia kuvuna kilo mia mbili au mia tatu tu, na ni kwa sababu tunadhani matatizo ya uzalishaji yanaweza kutatuliwa kisiasa”.

“Tulipowashauri wanunuzi, Gaki amekuwa mmoja wa wanunuzi waliowanufaisha zaidi wakulima wake, ambao sasa wanapata hadi kilo elfu moja sasa, tujiulize sisi ambao tuko mashambani, je, tunataka kufanya siasa au uzalishaji ambao utatuondoa kwenye umaskini?”

“Leo hii tunaye mkulima ambaye anapata kilo elfu moja kijiji A, lakini mkulima wa kijiji B ambapo tumeruhusu siasa ichukue nafasi anapata kilo mia mbili nasisitiza tena, tumeanza programu hii na tutaisimamia kwa nguvu sitakubali siasa kuchukua nafasi kwenye eneo la pamba tena, kwa sababu tayari tumeona matokeo hawa wanunuzi tuliwaambia wanunue matrekta mia moja, Gaki ametekeleza hilo”.

“Sisi, kama serikali, tumenunua matrekta mia nne kwa ajili ya zao la pamba lengo letu ni kuhakikisha kila kijiji kinacholima pamba kinakuwa na matrekta mawili yatakayosaidia shughuli za kilimo kwa wakulima wa maeneo hayo”.

Nitumie nafasi hii kukushukuru na kukupongeza wewe, Gaki, pamoja na wanunuzi wengine wa pamba nimewaambia pia wenzangu wa vyama vya ushirika kwamba huu ndiyo mwelekeo tunaopaswa kufuata lazima tuige mfano wa Gaki ili tuondokane na matatizo yaliyoko kwenye zao la Pamba."amesema Waziri Bashe

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo, ameishukuru serikali kwa msaada wake endelevu katika sekta ya kilimo, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi umekuwa na matokeo chanya katika uzalishaji wa pamba.

Kileo pia amebainisha kwamba, licha ya changamoto za mvua msimu huu, maeneo yenye maafisa ugani yamezalisha pamba ya kiwango bora na kwamba amepongeza vijana waliosimamia uzalishaji na ununuzi wa pamba kwa kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya kiwanda hicho.

"Msimu huu tulikuwa na mvua nyingi ambazo zilileta changamoto kwenye uzalishaji, lakini kwa maelekezo yako kupitia wizara yako, uliotuelekeza tuungane na serikali kuweka maafisa ugani, kuwawezesha kwa pikipiki, mafuta, na mishahara yao maeneo ambayo yamekuwa na maafisa ugani ndiyo yaliyofanikiwa kuzalisha pamba kwa ufanisi”.

“Kwa maelekezo yako, niseme tu kwamba bado tuna maafisa ugani 15 ambao wapo katika kata tatu kata ya Mbutu, Kishapu, na Meatu nakiri kabisa kuwa hizo kata zimezalisha vizuri sana kwa sababu walifuata maelekezo ya vijana uliowaleta kutoka chuo. Tumepunguza uchafu kwa asilimia kubwa sana baada ya vijana hao kusimamia zoezi la uzalishaji na pia zoezi la ununuzi wa pamba tumepata pamba ambazo zinakidhi mahitaji yetu kwa msimu huu."amesema Gasper Kileo

Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo akizungumza leo Septemba 12,2024 ambapo ameishukuru serikali kwa msaada wake endelevu katika sekta ya kilimo.

Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo akizungumza leo Septemba 12,2024 ambapo ameishukuru serikali kwa ushirikiano uliopo.

Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo akizungumza leo Septemba 12,2024 ambapo ameishukuru serikali kwa ushirikiano uliopo.

Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo akielezea mafanikio ya kiwanda hicho katika sekta ya Kilimo hasa zao la Pamba. 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akizungumza. 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohammed Bashe, Mkurugenzi wa Gaki Investment, Gasper Kileo wa kwanza upande wa kushoto na viongozi wengine wakielekea katika eneo la uchakataji wa Pamba ili kuona mafanikio kwenye kiwanda hicho.

Previous Post Next Post