Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kuimarisha juhudi zake za kuimarisha usalama kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vya usalama, kufanikisha operesheni mbalimbali za kudhibiti uhalifu.
Katika kipindi cha kuanzia Agosti 22 hadi Septemba 24, 2024, jumla ya watuhumiwa 55 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali, wakiwemo wahalifu waliokuwa wakijihusisha na biashara ya mafuta ya petroli, mali za wizi, na utengenezaji pombe haramu.
Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni mitungi 05 ya gesi, matairi mawili ya gari, pikipiki 05, pamoja na vifaa vya kielektroniki kama redio, boksi, na seti ya CCTV. Polisi pia wameweza kunasa lita 10 za pombe aina ya moshi, kompyuta mpakato moja, na vifaa vingine vya ramli chonganishi.
Aidha, kwenye mafanikio ya kesi mahakamani, jumla ya kesi 19 zimemalizika kwa ushindi, zikiwemo kesi za ulawiti, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, na matumizi ya madawa ya kulevya.
Kwa mfano, mshatakiwa wa kesi ya ulawiti amehukumiwa kifungo cha maisha jela, wakati wahusika wengine wa makosa kama kubaka na wizi walihukumiwa vifungo vya kati ya miaka 13 hadi 30.
Katika oparesheni za barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeweza kugundua makosa 5,048, kati yake 3,460 yalihusisha magari na 1,588 yalihusisha pikipiki, ambapo wahusika walilipa faini papo hapo.
Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano 41 na vikundi vya ulinzi shirikishi, vikilenga kuimarisha usalama barabarani na kuhakikisha kuwa waendesha bodaboda wanazingatia sheria pamoja na hayo, bodaboda wamepatiwa mafunzo maalum ya kuendesha vyombo vya moto kwa usalama ili kuepusha ajali barabarani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za nchi.