Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA SIASA CCM YAWATAKA WATUMISHI IDARA YA AFYA KUONGEZA USIMAMIZI WA FEDHA

Na Maria Antony,  SAME 

KAMATI ya siasa ya chama cha mapinduzi  imewataka watumishi katika idara ya afya kuongeza usimamizi  wa  fedha  zinazoletwa na serikali     kwa ajili ya  maendeleo na kudai kuwa Chama cha Mapinduzi na Serikali hakitamvumilia mtu yeyote atakayetumia fedha hizo vibaya. 


Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (MNEC) kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Seleman Mfinanga wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa mkoa wa Kilimanjaro wilayani Same. 


Mjumbe huyo akiongozana na jopo lake alitembea mradi wa uboreshaji wa kituo cha Afya Hedaru unaogharimu Fedha milioni 728 pamoja na mradi wa ujenzi wa zahanati ya Suji malindi ambapo unagharimu milioni 470.26.



Mfinanga alisema kuwa, lengo la Serikali  ni kuhakikisha huduma zinazogea karibu zaidi na wananchi na kuwataka Watumishi wa Umma kuhakikisha lengo la Rais linatimia kwa vitendo. 


Katika hatua nyingine kiongozi huyo aliwataka Watumishi kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi kwa vitendo na kufuata kanuni zinazowaongoza katika kazi. 


Aidha amewataka kuhakikisha fedha zinapoletwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitumike kwa wakati na kuzingatia pia thamani ya fedha ili wananchi wanufaike na fedha za Serikali. 


Akisoma taarifa ya uboreshaji kituo cha Afya Hedaru, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Benethson Rutahindurwa alisema kuwa, mradi huo umeibuliwa kwa lengo la kuboresha na kuongeza upatikanaji wa huduma ya Afya hususani za upasuaji, kuhifadhi miili na kutoa huduma ya X-ray. 


Alisema kuwa, kituo hicho cha Afya kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa Watumishi wakiwamo mtaalam wa mionzi na Daktari anaefanya upasuaji kwa sasa ni mmoja pamoja na wauguzi. 


Aidha Mganga Mfawidhi huyo alisema kuwa, kukamilika kwa jengo la mionzi kutaondoa adha kwa wananchi zaidi ya 40630 ambao wanatembea zaidi ya kilomita 50 kwa ajili ya kupata huduma hospitali ya wilaya ya Same.


Mwisho







Post a Comment

0 Comments