Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndg. Ally Hapi, anatarajiwa kufanya ziara rasmi katika mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 1 Oktoba hadi tarehe 6 Oktoba 2024. Ziara hiyo inalenga kuimarisha mshikamano na kushughulikia masuala ya wazazi ndani ya chama hicho.
Ndg. Hapi atafuatana na viongozi wengine muhimu wa mkoa, akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, Cde. John Siagi, na Katibu wa Wazazi Mkoa wa Shinyanga, Bi. Regina Ndulu.
Katika kipindi cha siku sita za ziara hiyo, Katibu Mkuu atafanya mikutano na wanachama wa Jumuiya hiyo, pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wazazi katika jamii, hasa katika maeneo ya elimu, afya, na maendeleo ya watoto.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Umoja wa Wazazi Tanzania kuhakikisha kuwa wazazi wanaendelea kuwa na nafasi ya kipekee katika kufanikisha malengo ya maendeleo ndani ya chama na taifa kwa ujumla.