KATIBU WA SMAUJATA KANDA YA ZIWA AKUTANA NA ASKOFU MKUU WA KANISA LA ORTHODOX NCHINI TANZANIA, WAPANGA MIKAKATI YA KUKOMESHA UKATILI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kanda ya Ziwa, Daniel Patrick Kapaya, amekutana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Orthodox nchini Tanzania, Francis Laurent Bukombe, maarufu kama Bludah, leo katika ofisi za SMAUJATA mkoani Shinyanga.

Mazungumzo hayo yameangazia kuimarisha ushirikiano katika kupambana na ukatili wa kijinsia, hususan dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bwana Kapaya ameainisha mafanikio na changamoto zinazoikabili SMAUJATA katika utekelezaji wa majukumu yake ambapo miongoni mwa changamoto alizozitaja ni ukosefu wa usafiri na vifaa vingine muhimu kwa ofisi za jumuiya hiyo mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake, Askofu Bukombe amepongeza juhudi za SMAUJATA katika kupinga ukatili wa kijinsia, ikiwemo ubakaji na ulawiti, huku akisisitiza kuwa kanisa lake litaendelea kushirikiana na SMAUJATA katika mapambano hayo. "Tutafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha tunapambana na vitendo visivyompendeza Mungu ili kuimarisha  amani na usalama wa jamii," amesema Askofu Bukombe.

Katika hatua nyingine, Askofu huyo ameahidi kusaidia kutatua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya SMAUJATA, ili kurahisisha kazi za viongozi wa jumuiya hiyo.

Aidha, Askofu Bukombe ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wake mzuri na viongozi wa dini, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa maslahi ya jamii.

Katibu wa SMAUJATA kanda ya ziwa Bwana Kapaya kwa amemshukuru Askofu Bukombe kwa msaada aliouahidi, ambapo amesema kuwa SMAUJATA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kanuni za nchi.

Jumuiya ya SMAUJATA inatekeleza majukumu yake chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, ambayo inaongozwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima.

Mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanaendelea kuwa ajenda ya kipaumbele kwa SMAUJATA, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda haki za kila mmoja katika jamii.

Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kanda ya Ziwa, Daniel Patrick Kapaya, akimpokea Askofu Mkuu wa Kanisa la Orthodox nchini Tanzania, Francis Laurent Bukombe, baada ya kuwasili katika ofisi ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 11,2024.

 

Previous Post Next Post