MAFANIKIO YA SHULE YA O.L.A ENGLISH MEDIUM YAVUTIA KATIKA MAHAFALI YA DARASA LA SABA NA AWALI 2024

Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa meneja wa Azania Benki tawi la Kahama, Afisa mwandamizi wa Kilimo katika Benki hiyo, Agnes Kidugo akiipongeza shule ya msingi O.L.A

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shule ya Awali na Msingi Our Lady of Apostles  (Mama yetu wa Mitume) O.L.A iliyopo kata ya Didia, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, imefanya mahafali yake ya nne ya darasa la saba na ya 11 kwa wanafunzi wa awali, ikijivunia mafanikio makubwa katika nyanja za kitaaluma, kijamii, na kimaadili.

Sherehe hizo zimefanyika Septemba 28, 2024, katika ukumbi wa shule hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Mthibiti Ubora wa Shule kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Diwani wa kata ya Didia.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, ambaye ni mwakilishi wa Meneja Bank ya Azania  tawi la Kahama, Agnes Kidugo, amewasisitiza wahitimu waendelee kuwa watiifu, wachapa kazi, na kushikilia maadili mema.

Pia amewasihi wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa shule yao ya O.L.A, huku akiwapongeza kwa juhudi walizoweka katika masomo yao.

 “Niwasihi wahitimu mkaendelee kuwa mabalozi wazuri wa O.L.A yale yote mliyofundishwa katika shule hii msiyaache hapa hapa ila muende nayo mkawe mabalozi huko muendako Dunia sasa hivi inachangamoto nyingi sana nawasihi mkawe mfano mzuri katika jamii, natumaini mtafaulu vizuri na huko muendako katika elimu yenu ya sekondari mkatie bidii, kama mlivyokuwa mkifanya hapa O.L.A ili muweze kufika elimu ya juu na hatimaye mkawe na mchango mkubwa katika taifa la Tanzania na nje ya nchi’.

Mkuu wa shule hiyo, Sister Comfort Yawa Amevor, amewahakikishia wazazi kuwa wahitimu wamepata elimu bora itakayowawezesha kufaulu katika hatua zao zinazofuata.

 Ameeleza kuwa mafanikio ya shule yamechangiwa sana na ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, na wazazi, akisisitiza kuwa shule hiyo haina lengo la kufundisha tu masomo bali pia maadili mema.

 “Hii shule hatufundishi tu taaluma pia tunafundisha maadili mema na ujuzi wetu baada ya mitihani huwa tuna muda wa kujifunza kwa vitendo hapa O.L.A matokeo siyo ya mwalimu matokeo niya mtoto mwenyewe kama mtoto anapata A maana yake amepata uelewa mkubwa darasani tumewafundisha watoto kujitegemea wenyewe kwenye mitihani kwahiyo leo tunawatuma kwenda kuwa mabalozi waziri wa O.L.A”.

“Kwa upande wa ushirikiano kwa kweli tunapata ushirikiano sana kwa kila mmoja wazazi pamoja na bodi ya shule wapo na sisi muda wote kwahiyo tunawashukuru sana mungu awabariki tunaomba ushirikiano huu uendelee”.amesema Sr. Comfort

Katika risala ambayo imesomwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi Yohana Thomas Shija, amebainisha kuwa shule hiyo imeonyesha ongezeko kubwa la ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo, ikiendelea kujenga msingi bora wa kitaaluma kwa wanafunzi wake.

Katika kipindi cha miaka kadhaa, shule ya O.L.A English Medium imeendelea kujijengea sifa kubwa kutokana na mafanikio yake makubwa kitaaluma na kijamii.

Mafanikio haya yamekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya Kahama, mkoa wa Shinyanga, huku shule ikijipambanua kama moja ya taasisi zinazotoa elimu bora.

Moja ya sehemu kubwa ya mafanikio ya shule ya O.L.A ni ukuaji wa viwango vya taaluma ambapo amesema kwa miaka mitatu mfululizo, shule imeonyesha ongezeko kubwa la ufaulu kwenye mitihani ya taifa (PLSE), ambapo mwaka 2021 kati ya wanafunzi 33 waliofanya mtihani, 10 walipata daraja A, 22 daraja B, na mmoja alipata daraja C, na wastani wa ufaulu ulikuwa 227.

Mwaka 2022, shule ilipanda hadi wastani wa ufaulu wa 256, ambapo wanafunzi 17 walipata daraja A na 4 walipata daraja B, na kwamba mwaka 2023, ufaulu ulikuwa juu zaidi na wastani wa ufaulu wa 261, ambapo kati ya wanafunzi 26 waliofanya mtihani, 23 walipata daraja A na watatu walipata daraja B.

Mafanikio haya ya kitaaluma si tu yanahusisha mitihani ya darasa la saba bali pia yanaendana na uwezo wa shule kuwapeleka wanafunzi wake kwenye shule maalumu kitaifa ambapo Shule ya O.L.A imefanikiwa kupeleka wanafunzi bora 21 waliochaguliwa kujiunga na shule za vipaji maalum, shule za ufundi, na shule za kitaifa za bweni hii ni ishara ya kujituma kwa walimu na wanafunzi, pamoja na ushirikiano wa karibu na wazazi.

Aidha, shule imeendelea kuwekeza katika michezo, sanaa, na kazi za mikono ili kuwajengea wanafunzi umahiri wa ziada nje ya masomo ya darasani, kwa kufanya hivyo, shule ya O.L.A inakuwa chachu ya kuibua vipaji vya kipekee na kuandaa watoto wenye ujuzi wa kushindana kwenye masoko ya ajira na maisha kwa ujumla.

Historia Fupi ya Shule

Shule ya O.L.A English Medium ilianzishwa tarehe 4 Februari, 2013, na Masista Wamisionari wa Shirika la Mama Yetu wa Mitume (Our Lady of Apostles - O.L.A.).

Hapo awali, shule ilianza na wanafunzi 50 kwenye ngazi ya elimu ya awali pekee, chini ya uongozi wa Mwalimu Mkuu mwanzilishi Sr. Rita Dung, tangu wakati huo shule imeendelea kukua kwa kasi na sasa ina jumla ya wanafunzi 334, ambapo wavulana ni 166 na wasichana ni 168 Shule pia ina jumla ya wafanyakazi 39, wakiwemo walimu 17, wafanyakazi wasio walimu 20, na Masista wawili.

Shule ya O.L.A pia imejivunia kumpokea Mwalimu Mkuu mpya Sr. Comfort Amevor, ambaye ameendelea kushikilia misingi imara iliyowekwa na viongozi wa awali wa shule.

Wahitimu wa mwaka huu, walionza darasa la kwanza mnamo mwaka 2018, walikuwa na idadi ya wanafunzi 51, lakini waliomaliza safari yao ya elimu ya msingi ni wanafunzi 27 pekee, kati yao wavulana 17 na wasichana 10.

Baadhi ya wahitimu wa shule ya O.L.A wamemshukuru Mungu kwa kumaliza masomo yao ya darasa la saba na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo, wakitarajia matokeo mazuri katika mitihani yao ya kitaifa.

 Nao baadhi ya wazazi na walezi waliohudhuria mahafali hayo, wameipongeza Shule ya O.L.A kwa ufaulu mzuri wa wanafunzi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ambapo wamesema kuwa juhudi za walimu pamoja na mazingira bora ya kujifunzia yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya wanafunzi.

Wameongeza kuwa shule hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika kukuza taaluma na maadili kwa watoto wao, na wanatarajia matokeo mazuri zaidi katika miaka ijayo.


Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Meneja wa  Benki ya 

Azania tawi la Kahama, Afisa mwandamizi wa Kilimo katika Banki hiyo, Agnes Kidugo akizungumza kwenye mahafali shule ya msingi O.L.A 2024.


Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Meneja wa  Benki ya 

Azania tawi la Kahama, Afisa mwandamizi wa Kilimo katika Banki hiyo, Agnes Kidugo akizungumza kwenye mahafali shule ya msingi O.L.A 2024.


Mkuu wa shule ya O.L.A Sister Comfort Yawa Amevor, akiwahakikishia wazazi kuwa wahitimu wamepata elimu bora itakayowawezesha kufaulu katika hatua zao zinazofuata.

Mkuu wa shule ya O.L.A Sister Comfort Yawa Amevor, akiwahakikishia wazazi kuwa wahitimu wamepata elimu bora itakayowawezesha kufaulu katika hatua zao zinazofuata.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Yohana Thomas Shija, akisoma taarifa fupi ya shule hiyo katika mahafali Septemba 28, 2024. 

Mgeni rasmi akitoa zawadi baada ya burudani kwa wanafunzi wa shule ya msingi O.L.A










 

Previous Post Next Post