Na Mapuli Kitina Misalaba
Tarehe 23
Agosti 2024 itabaki kuwa siku ya kukumbukwa kwa Daniel Patrick Kapaya,
alipochukua rasmi majukumu ya kuwa Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na
Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kwa Kanda ya Ziwa.
Baada ya kuteuliwa, Kapaya ameahidi kwa sauti kubwa
kupambana na ukatili katika kanda hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano
wa karibu na viongozi wa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi
kwa ujumla.
Shukrani
kwa Uongozi wa Taifa: "Mwenyekiti Sospeter Bulugu na Viongozi Wengine
Wameniamini"
Kapaya alitumia fursa ya siku hiyo kutoa shukrani
zake za dhati kwa uongozi wa taifa wa SMAUJATA, akianza na Mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo, Sospeter Bulugu, ambaye alifanya uamuzi wa kumteua yeye kama
Katibu wa Kanda ya Ziwa.
"Nitumie
fursa hii kuushukuru uongozi wangu wa taifa, nikianza na Mwenyekiti wangu
Sospeter Bulugu aliyeniteua kuwa Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, pamoja na
waandamizi wake akiwemo Kamishna Hashim Omary na viongozi wengine waandamizi
kwa kuniona nafaa kusimamia Kanda ya Ziwa,"
alisema Kapaya kwa furaha.
Aliendelea kwa kusema, "Nisema tu kwamba katika kuniteua huku hawajakosea nitapambana
katika mikoa yangu sita na nitafanya kazi kwa uadilifu nitatembea kila mkoa
kuhakikisha ukatili uliopo tunaweza kuumaliza, pia nitahakikisha viongozi wa
mikoa yangu wanafanya kazi kwa haraka zaidi katika kuwafikia wahanga wanaopata
ukatili wa kijinsia."
Katika hotuba yake, Kapaya alisisitiza kuwa SMAUJATA
inafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalum, ambayo inaongozwa na Dkt. Dorothy Gwajima.
Alisema, "Niishukuru Wizara ya Maendeleo ya
Jamii ambayo tunafanya nayo kazi kwa pamoja, inayosimamiwa na Dkt. Dorothy
Gwajima kwa ukaribu kabisa yupo bega kwa bega na SMAUJATA, na SMAUJATA inafanya
kazi kwa moyo mmoja ikiona kabisa wizara hii inatupa ushirikiano."
Kapaya aliwahimiza maafisa ustawi wa jamii, maafisa
maendeleo ya jamii, na Dawati la Jinsia kushirikiana nao kikamilifu huku akiendelea
kuomba viongozi wa mikoa yao kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na
SMAUJATA kwa lengo la kutokomeza ukatili.
"Niombe
basi viongozi waliopo katika mikoa yetu waweze kusimama na sisi bega kwa bega
kama Waziri Dorothy Gwajima anavyopambana na SMAUJATA,".alisema Kapaya
Vipaumbele
vya Kapaya katika Kanda ya Ziwa: "Kupambana na Ukatili na Kutoa Haki kwa Makundi
Maalum"
Kapaya aliweka wazi kuwa moja ya vipaumbele vyake
kuu itakuwa ni kuhakikisha haki za msingi zinatolewa hasa kwa watoto, wanawake,
vijana, na watu wenye ulemavu ambao ni makundi maalum katika maeneo yao.
Alizungumza kwa uchungu kuhusu suala linalotrendi
kwenye mitandao ya kijamii la utekaji wa watoto, akisema, "Kwa kweli hatuna raha kama SMAUJATA, mimi kama kiongozi wa kanda
nitaweza kulisimamia pamoja na viongozi walioko kwenye mikoa walifanyie kazi
haraka kweli."
Kipaumbele kingine cha Kapaya ni kutembelea maeneo
ya migodi katika Kanda ya Ziwa, ili kuhakikisha utekelezaji wa sera
zinazozungumzia kuzuia ukatili wa kijinsia.
Alisema, "Kuna
watoto wanaajiriwa katika umri mdogo, lakini vile vile tunaangalia na
unyanyasaji wa kwenye migodi pengine kuna watu hawapati haki zao za msingi kama
Katibu wa Kanda ya Ziwa, nitaweza kufanya hivyo na niwaombe tu viongozi wa
mikoa nitakapoanza kufanya ziara zangu waweze kuniandalia sehemu zenye migodi
tupite kwa ajili ya kuangalia utekelezaji wa sera zinazozungumzia kuzuia
ukatili wa kijinsia."
Elimu
ya Ukatili wa Kijinsia na Utengenezaji wa Timu ya Mashujaa: "Tuzidishe
Ushirikiano ili Tupambane na Ukatili"
Kapaya pia alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya
ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kuwa kila mkoa unajenga timu kubwa ya
mashujaa wanaopinga ukatili.
Alisema,
"Naiomba kila mkoa uhakikishe imetengeneza timu kubwa ya mashujaa waeleweke
kwenye data bezi ya SMAUJATA lengo kubwa ni kupunguza uhalifu wa vitendo vya
ukatili."
Kwa kumalizia, aliomba serikali iweze kutoa
ushirikiano kwa viongozi wa SMAUJATA, hasa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao
katika ngazi za chini. "Niwaombe
sana maafisa ustawi wa jamii, maafisa maendeleo ya jamii, na Dawati la Jinsia
mnapoona shujaa amekuja kiongozi wa SMAUJATA mmpe ushirikiano ili awe na moyo
wa kufanya kazi," alihimiza.
Ahadi
ya Kapaya kwa Kanda ya Ziwa: "Nipo Bega kwa Bega Kupambana na
Ukatili"
Kapaya alihitimisha hotuba yake kwa kuahidi kutoa
ushirikiano wakati wote kwa wananchi na viongozi wa SMAUJATA katika Kanda ya
Ziwa. Alisema, "Ninaahidi kutoa
ushirikiano wakati wote endapo kuna matatizo yoyote ya ukatili msisite
kunijulisha, mimi nipo bega kwa bega na nitafanya kazi muda wowote na saa
yoyote pindi mtakaponihitaji."
Aidha, alitoa shukrani maalum kwa Mkoa wa Shinyanga
kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati alipokuwa Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa
Shinyanga alisema, "Kwa kweli tumefanya kazi vizuri na tumeweza kupambana
na ukatili tukishirikiana na viongozi wangu wa SMAUJATA kwa kweli, ukatili Mkoa
wa Shinyanga umeweza kupungua."
Maombi kwa Wazazi: "Wachungeni Watoto,
Tupunguze Vitendo vya Utekaji"
Kapaya alimaliza kwa kuwasihi wazazi kuchukua hatua
madhubuti katika kuwalinda watoto wao. Alisema, "Nipande tu kuwaasa wazazi sasa wakae vizuri na watoto, wawe
wanawachunguza na kuwalinda ili tupunguze vitendo vya utekaji pia watoto wapate
elimu, lishe bora, na mafundisho ya kidini ili wakue wakiwa na hofu ya
Mungu."
Kwa ujumla, Daniel Patrick Kapaya anaonekana kuwa na
nia thabiti ya kuleta mabadiliko makubwa katika mapambano dhidi ya ukatili
katika Kanda ya Ziwa, huku akihimiza ushirikiano wa kila mmoja katika
kuhakikisha jamii inakuwa salama na yenye haki.
Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii
Tanzania (SMAUJATA) ni jumuiya ya kupinga ukatili nchini inayotekeleza majukumu
yake chini ya wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum.