Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Iddi Kassim Iddi, leo ameshiriki katika mahafali ya shule ya Sekondari Bulige, ambapo ameahidi kuchangia kompyuta tano pamoja na kutoa shilingi milioni moja kwa ajili ya kununua viti na meza za walimu.
Katika hotuba yake, Mhe. Iddi alisisitiza umuhimu wa elimu kwa wanafunzi na akawataka wazazi kuhakikisha wanawasimamia watoto wao ili waweze kuhudhuria masomo bila kukosa. Alieleza kuwa utoro wa wanafunzi ni changamoto inayokwamisha maendeleo ya elimu na juhudi za kuinua ubora wa shule katika jamii.
"Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anahudhuria masomo kwa wakati. Elimu ndiyo msingi wa maendeleo, na hatuwezi kufikia malengo yetu kama watoto wetu hawahudhurii shule," alisema Mhe. Iddi Kassim.
Wanafunzi, walimu na wazazi waliohudhuria mahafali hayo walimshukuru Mbunge kwa msaada wake na juhudi zake katika kuimarisha mazingira ya elimu katika jimbo hilo.