MTANDAO WA KUPINGA NDOA ZA UTOTONI NA ZIARA YAO YA KISHINDO MIKOA MINNE.

Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Mimba za Utotoni, Lilian Kimati akizungumza kwenye mkutano wa kutoa elimu ya namna ya kupambana na mimba hizo za utotoni uliofanyika mkoani Mara.

Na Elizabeth Cornely, SHINYANGA

MTANDAO wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania(TECMN), unaojumuisha mashirika ya kiraia zaidi ya 80 unafanya ziara katika mikoa minne ya Mara, Shinyanga, Tabora na Dodoma kutoa elimu juu ya kupambana na ndoa za utotoni nchini.

Miongoni mashirika hayo, Msichana Initiative, Medea, Plan International na My Legacy ndio yamewakilisha mashirika mengina katika ziara hiyo maalumu kwenye mikoa hiyo minne.

Lengo kubwa la ziara hiyo mbali na kutoa elimu juu ya kupambana na kutokomeza ndoa hizo za utotoni,  pia inaikumbusha serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hususani kwenye vifungu vya 13 na 17 vinavyoruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au kwa amri ya mahakama.

Ikumbukwe kwamba Rebecca Gyumi ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, alifungua kesi  Mahakama Kuu ya Tanzania kwa niaba ya watoto wote walio katika hatari ya kuingia kwenye ndoa za utotoni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali la madai namba tano(5) ya mwaka 2016 kupinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za utotoni.


Rebecca alishinda shauri hilo baada ya mahakama hiyo kutamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume cha Katiba na kwamba vimepitwa na wakati.

Alipinga vifungu hivyo vya 13 na 17 kwa misingi kwamba vinakiuka ibara ya 12(1)ya  Katiba ya Tanzania inayotoa usawa kwa watu wote mbele ya sheria.

Pia, alipinga kwamba vifungu hivyo vinakiuka ibara ya 13(1)(2) ya Katiba hiyo ya nchi ambayo inawalinda watu dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya kijinsia, ambayo kadhalika inaeleza kwamba watu wenye umri chini ya miaka 18 ni watoto na hawana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi juu kuoa au kuolewa.

Alipinga kuwa vinakiuka ibara ya 21(2) ya Katiba hiyo kwa kutowapa wasichana fursa ya kushiriki kikamilifu katika kuamua mustakabali wa maisha yao na kwamba vinamnyima mtoto haki ya kupata elimu na uhuru wa mawazo.

Hukumu inasemaje

Mahakama hiyo Kuu Julai 8 mwaka 2016, ilitoa hukumu ikitamka kuwa, ndoa yoyote ya mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ni kinyume cha sheria na kwamba vifungu hivyo vinaruhusu watoto kuingia kwenye ndoa wakati haifai kuwaingiza watoto katika majukumu makubwa ya ndoa na kuonyesha hatari zake kiafya inayowakabili watoto hao pale wanapoolewa wakiwa na umri mdogo.

Mahakama ilitoa uamuzi kwamba vifungu hivyo havitoi usawa kwa msichana na mvulana katika njia mbili, kwanza umri wa ndoa tofauti kati yao, pili, wasichana chini ya umri wa miaka 18 wanahitaji ridhaa ya wazazi kuolewa wakati wavulaa hawahitaji na kuonyesha kwamba tofauti hiyo inatoa maana kwamba wasichana na wavulana hawatendewi sawa chini ya vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa na kuonyesha ubaguzi na vinakiuka ibara ya 12 na 13 za Katiba ya nchi.

Hata hivyo, serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu, ilikata rufani kupitia shauri namba 204 la mwaka 2017 kupinga uamuzi huo wa mahakama Kuu lakini mwaka 2019 Mahakama ya Rufani ilimpatia tena ushindi Rebeca na kutoa mwaka mmoja sheria hiyo iwe imefanyiwa marekebisho.

Pamoja na amri hiyo ya mahakama, bado sheria hiyo haijafanyiwa mabadiliko.

Akizungumza jana kwenye ziara hiyo Tarime mkoani Mara, Mratibu wa Mtandao huo wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, Lilian Kimati, wanatamani ndoa hizo ziishe ili watoto wapate fursa ya kutimiza ndoa zao.

mwisho.



Previous Post Next Post