Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga
limefanikiwa kumkamata Paul Shija (19), mkazi wa kata ya Ndala, Manispaa ya
Shinyanga, kwa tuhuma za kumjeruhi Ester Matalanga (25), ambaye ni mkazi wa
eneo hilo.
Tukio hilo limemhusisha Shija, ambaye
alikuwa mume wa zamani wa Esther Matalanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, tukio hilo lilitokea
mnamo tarehe 13 Agosti 2024 ambapo Ester Matalanga alijeruhiwa kwa kutobolewa macho yake yote mawili na Paul
Shija, ambaye alikuwa mume wake wa zamani.
Jeshi la Polisi lilichukua hatua za
haraka kufika eneo la tukio, ambapo walimchukua Matalanga na kumpeleka katika
Hospitali ya Kolandoto, iliyopo Manispaa ya Shinyanga, kwa ajili ya matibabu ya
haraka.
Kamanda Magomi amesema kuwa
upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea, na mara baada ya kukamilika, sheria
itachukua mkondo wake ili kuhakikisha haki inatendeka.
Aidha, Kamanda Magomi amewataka
wananchi waendelee kushirikiana na jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zinazohusu
wahalifu na uhalifu katika maeneo yao.
Ameweka wazi kuwa taarifa za kiintelijensia
kutoka kwa raia wema ndizo zilizosababisha mafanikio ya kukamatwa kwa mtuhumiwa
huyo, ambaye alikutwa nyumbani kwake kutokana na taarifa za siri kutoka kwa
wasamaria wema.
Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza
raia kuachana na tabia ya kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza kuwa hatua
kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika na vitendo vya aina
hiyo.
Tukio hilo limeibua hisia kali
miongoni mwa wakazi wa Shinyanga, wengi wakilaani kitendo hicho na kuitaka jamii
kuungana kupinga ukatili wa kijinsia.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu
upelelezi wa tukio hili na hatua zaidi kutoka kwa mamlaka husika, huku
tukilenga kutoa taarifa za kina kwa wananchi kupitia MISALABA MEDIA.