MWENYEKITI WA MACHIFU TANZANIA ANTONIA SANGALALI AADHIMISHA MIAKA 18 YA UONGOZI WA KIMILA HIMAYA YA JIGOKU, RAIS SAMIA ATAJWA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Chifu Antonia Sangalali Matalu, Ntemi wa Himaya ya Jigoku katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, na Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania (U.M.T), ameandaa tamasha kubwa la kiutamaduni na kuhimiza jamii kuenzi mila, desturi, na utamaduni wa Kitanzania.

Tamasha hilo limefanyika Septemba 15, 2024 katika Kata ya Masela, Himaya ya Jigoku, likihudhuriwa na viongozi wa kimila, serikali, mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, na wadau mbalimbali, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza katika tamasha hilo, Chifu Antonia amesema kuwa, urithi wa kitamaduni ni nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye maadili bora, hasa kwa vizazi vya sasa na vijavyo ambapo amewasihi wazazi na walezi kuwalea watoto wao kwa kufuata maadili yanayozingatia mila na desturi nzuri za Kitanzania

 "Wazazi na walezi mnapaswa kuwalea watoto wenu kwa kuzingatia maadili bora yanayopatikana kwenye mila zetu," amesema Ntemi Antonia

Amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa chakula ili kuepuka baa la njaa na kwamba amewahimiza wananchi hao kuendelea kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya jamii.

Pia, Ntemi Antonia amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025, huku akiwapongeza kwa ushiriki mzuri kwenye zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

“Nikiwa kama mwenyekiti wa Machifu Tanzania, niwahimize tutunze chakula ili kuepuka njaa katika familia zetu, na tushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao," amesema Chifu Antonia.

Kwa upande mwingine, Ntemi Antonia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuenzi na kulinda mila na desturi za taifa ambapo amebainisha kuwa Rais Samia ni kiongozi wa mfano anayefanya maamuzi sahihi kwa kushirikiana na viongozi wengine.

"Rais wetu anaheshimiwa duniani kote ni kiongozi wa maamuzi makubwa na sisi Wasukuma tunampenda, tunamheshimu na kumwona kama nyota ya asubuhi,"

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge, amempongeza Chifu Antonia kwa mchango wake katika kulinda mila na desturi, akibainisha kuwa serikali inatambua na kuthamini juhudi zake.

“Chifu Antonia amekuwa kiunganishi muhimu kati ya serikali na jamii za kimila tunajivunia kuwa na kiongozi wa kimila kama yeye," amesema Kaminyoge.

Pia, amesisitiza juu ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kuhara na kutapika, ambapo amehimiza wananchi kuhakikisha usafi wa mwili na mazingira ili kuepuka maambukizi ya kipindupindu.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Misalaba Media wamempongeza Chifu Antonia kwa kuendeleza tamasha la kiutamaduni, huku wakiahidi kuendeleza mila na desturi za eneo hilo kwa vizazi vijavyo.

Tamasha hilo lililoongozwa na kauli mbiu “TULINDE MILA NA TAMADUNI ZETU” limepambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa ngoma na nyimbo za asili, akiwemo Nelemi Mbasando na Ng’wana Kang’wa.

Kwa ujumla, kumbukizi ya miaka 18 ya makumbusho ya Himaya ya Jigoku katika utawala ya Ntemi Antonia Sangalali imeacha historia ya kipekee kwa wakazi wa Maswa na Mkoa wa Simiyu ambapo tamasha hilo limekuwa kielelezo cha umuhimu wa kuenzi na kudumisha urithi wa kitamaduni kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa kutumia fursa hii, viongozi wamehamasisha watu kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, kisiasa, na kiutamaduni, ili kudumisha mshikamano na maendeleo katika jamii yao.

Chifu Antonia akiwapongea viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge kwa ajili ya kushiriki katika tamasha hilo.

Chifu Antonia Sangalali Matalu, Ntemi wa Himaya ya Jigoku katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, na Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania (U.M.T), akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni 2024.

Chifu Antonia Sangalali Matalu, Ntemi wa Himaya ya Jigoku katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, na Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania (U.M.T), akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni 2024.

Wananchi wakifuatilia tamasha la utamaduni Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, kumbukizi ya Miaka 18 ya makumbusho himaya ya Jigoku ya Ntemi Antonia Sangalali.




Previous Post Next Post