Na Bora Mustafa,
Misalaba Media, Arusha.
Wadau wa maendeleo wamekumbushwa kuwa ili kuchochea uchumi wa viwanda ni lazima kuwekeza katika umeme wa uhakika.
Hayo yamezungumzwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo leo wakati akifungua wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI).
Amesema ili kuelekea dira ya maendeleo 2050 serikali imeendelea kuweka nguvu katika nishati ya umeme kwani ni nishati inayotegemewa katika uzalishaji nchini hasa kwenye sekta ya viwandaa.
Aidha amewataka wananchi kupatiwa mazingira bora na huru ya kufanya biashara ,ndani ya nchi na nje ya nchi ili kujikwamua kiuchumi pamoja na kuweza kushiriki katika soko la ushindani.
Amesema Tanzania imelenga baada ya miaka 25 ijayo isiwe na watu maskini na hivyo itahakikisha inaendelea kuendeleza ustawi wa watu wake hususani katika elimu.
"Inabidi kuwe na uwekezaji katika elimu ,watu wanatakiwa wajue kusoma na kuandika kwani mpaka sasa nchini kwetu asilimia 75 hadi 80 wanajua kusoma na kuandika kwa upande wa elimu ya msingi lakini pia kwa upande wa elimu ya sekondari ,serikali imefikia asilimia 75" amesema Prof. Mkumbo.
Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society Justice Rutenge amesema wanahitaji kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi katika nyanja mbalimbali mfano elimu, afya, kilimo ili kufikia mahali ambapo kama nchi inahitaji kufika.
Mkuu wa Sekta ya Umma kutoka Benki ya Stanbic Doreen Dominic amesema lengo la mkutano huo ni kuweka mustakabali endelevu na jumuishi na kuleta matumaini kwa watanzania wote kuelekea kutimiza malengo ya maendeleo ya Taifa 2050.