Na Elizabeth Zaya
SERIKALI imeelekeza kiasi cha Sh. bilioni 81 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mbambabay Wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema ujenzi wa bandari hiyo ukikamilika utasaidia kutoa ajira, kuinua Uchumi, kupeleka na kupokea bidhaa mbalimbali ikiwemo mazao, samaki na bidhaa za viwandani katika Nchi Jirani za Malawi na Msumbiji.
Ameyasema hayo akiwa ameambatana na kamati ya usalama ya Mkoa huo kwenye ziara ya kukagua miradi katika utayari wa mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajia kuanza ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma hivi karibuni ambapo pia atakuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Mjini Songea kuanzia Septemba 20 hadi 23 mwaka huu.