Na Mapuli Kitina Misalaba
Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa
Jamii Tanzania (SMAUJATA), Mkoa wa Shinyanga, imeliomba jeshi la polisi mkoani
Shinyanga kumkamata mwanaume anayedaiwa kumjeruhi mke wake kwa kumpiga na mpini
wa jembe kichwani.
Tukio hilo limetokea Septemba 23, 2024 majira
ya saa nne usiku katika mtaa wa Bugweto, Manispaa ya Shinyanga.
Viongozi hao wametoa wito huo walipomtembelea
mwanamke huyo ambaye amelazwa katika zahanati binafsi ya Bugweto na kwamba Mwanamke
huyo amelazwa kwa matibabu baada ya kujeruhiwa, huku viongozi wa SMAUJATA
wakishinikiza mwanaume huyo aitwaye Stevin Silas akamatwe na kuchukuliwa hatua
kali za kisheria.
Mwanamke huyo ameeleza kuwa amekuwa
akifanyiwa ukatili na mwanaume huyo, ikiwa ni pamoja na kulawitiwa ambapo
amesema kuwa licha ya kesi ya ulawiti kuwa inaendelea, mwanaume huyo aliendelea
kumsumbua, na hatimaye akampiga kwa mpini wa jembe kichwani alipokuwa akirudi
nyumbani kutoka kazini.
"Nilikuwa
natoka kazini usiku, nikamuona akiwa na mpini wa jembe, lakini sikutilia
maanani alinisubiria nyumbani na aliponiona alinipiga kichwani nikadondoka huku
nikiwa nimembeba mtoto mgongoni,"
amesema mwanamke huyo.
“Nilikuwa
na mwenza wangu nimeishi naye zaidi ya Mwaka mmoja ila kuna migogoro imetokea alikuwa
akiniingia sehemu za kinyume na maumbile yangu nilienda kwenda kuripoti kituo
cha polisi alikamatwa akakaa polisi siku tano badaye alienda kutolewa dhamana
na baba yake mdogo tukawa hatuwasiliani naye mimi nilipanga kwenye chumba
changu baada ya hapo akawa ananifuatilia tukio la pili nilikuwa natoka kazini
saa nne usiku wakati natoka kazini nay eye nilimuona anafunga kwenye kazi yake
huwa anafanya kazi ya saloni kunyoa watu nilimuona akiwa ameshikiria mpini
lakini sikumfuatilia wakati nafika nyumbani kumbe yeye alitangulia akaenda
kukaa sehemu kunisubiria nilipofika nyumbani kabla zijaingia getini nikasikia
mtu anakimbia nikageuka nikamuona akanipiga mpini wa jembe kichwani nikadondoka
nilikuwa nimebeba mtoto mgongoni yeye alikimbia”.ameeleza
mwanamke huyo
Kwa upande wake, Dkt. Mathias Ndega, daktari wa zamu
aliyempokea mwanamke huyo katika zahanati ya Bugweto, amesema walimpokea
mgonjwa akiwa anatokwa na damu nyingi kichwani ambapo ameeleza hali ya
mgonjwa kuwa ni ya kuridhisha baada ya kumpatia matibabu ya jeraha kubwa
kichwani.
"Tuligundua
jeraha lake ni kubwa na tulilazimika kumshona nyuzi 12 kwa sasa hali ya mgonjwa
inaendelea vizuri," amesema Dkt.
Ndega
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana
Daniel Kapaya, amelaani vikali kitendo hicho, akisema ni ukiukwaji wa haki za
binadamu na ukatili mkubwa ambapo ameliomba jeshi la polisi kumkamata mtuhumiwa
haraka na kumfikisha mbele ya sheria.
“Tumepokea
taarifa ofisi ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwamba kuna mwanamke amepata
shambulio basi ofisi ya SMAUJATA tumefika kumwona huyu dada nan i kweli baada
ya kufika hapa tumemuona huyu dada kweli amepata majeraha makubwa kichwani,
sasa tumeona kama sisi SMAUJATA hili suala la watu kuwaruhusu mfano kama huyu
aliyefanya ukatili wa kulawiti ametoka tu polisi hajamaliza hata wiki mbili
amefanya tena shambulio lingine tunaona ni ukatili mkubwa sana”.
“Ofisi
ya SMAUJATA inalaani sana na vitendo kama hivi mtu kama huyu alikuwa anafanya
shambulio la mauaji kwahiyo mimi katibu wa SMAUJATA kanda ya ziwa ninalaani
sana vitendo kama hivi vya ukatili ambavyo vinaonekana kwenye jamii mimi
niiomba serikali hasa jeshi la Polisi waweze kumtafuta huyu mtuhumiwa au yule
aliyemdhamini kwa hatua ile ya kwanza ya ulawiti waweze kushikiliwa ili huyo
dada aweze kutoka hapa Hospitali ninaomba sana polisi waweze kumtafuta ili
kusudi huyo mtu aweze kupata adhabu yake”.amesema Kapaya
Mtendaji wa mtaa wa Bugweto, Bwana Joseph
Masalu, amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kuchukua hatua za kutoa
taarifa kwa jeshi la polisi.
Familia ya mwanamke huyo imeiomba serikali
kuhakikisha haki inatendeka, huku majirani wakielezea hofu yao kutokana na
matukio ya ukatili mkoani Shinyanga.