Ticker

6/recent/ticker-posts

TAMASHA LA UTAMADUNI LAWAKOSHA WAFANYABIASHARA RUVUMA



Na Elizabeth Zaya

BAADHI ya wakazi wa Songea mkoani Ruvuma wamefurahia ujio wa Tamasha la Kitaifa la utamaduni mkoni Ruvuma kwa kuwapa fursa za kufanyabiashara na kujitangaza kupitia tamasha hilo.

Kadhalika, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwa na tamasha la utamaduni kwa kuwa pamoja na kuwakumbusha kuenzi tamaduni zao lakini wanalitumia kujinufaisha kiuchumi.

Tamasha la Utamaduni la Kitaifa linatarajiwa kufanyika kwa mara ya tatu mkoani Ruvuma kuanzia Septemba 20 mpaka 23 na mgeni rasmi kwenye kilele chake ni Rais Samia.

Tito Mbilinyi, mkazi wa Songea mkoani Ruvuma, anasema matamanio yao kwa miaka mingi ilikuwa kuona tamaduni zao zinaendelezwa, hivyo wanampongeza Rais Samia kwa kuliona hilo na kuruhusu kufanyika.

“Mimi namshukuru sana Rais Samia kwa kutuletea tamasha hili, tulilisubiri sana, kwa hiyo tumefarijika sana,"anasema Mbilinyi.

Sisi kama wafanyabiashara tunasema hivi, karibu mgeni, mwenyeji apone, kwa sababu hata mwenye nyumba ya kulala wageni, mama lishe, anayejishughulisha na usafirishaji,wote tutanufaika kwa sababu ugeni utakaokuja ni mkubwa sana."

“Na haya ndiyo tulikuwa tunaomba miaka yote kwamba angalau viongozi wetu wa mkoa wawe wanatuletea fursa kama hizo, sisi tunasema tunampongeza sana Rais Samia, kwanza ametuelewa sana sisi sekta binasfi hasa katika biashara na nimsikivu kwa sababu  zile changamoto ambazo tumekuwa tukizilalamikia kwa miaka mingi naona ameanza kuzitatua, tunamshukuru sana.”

Alisema wakazi wa mkoa huo wamefurahi na wanasubiri kumpokea Rais Samia na wamejipanga kumuonyesha utajiri uliopo  katika mkoa huo.

“Rais wetu tunamkaribisha mkoa wa Ruvuma, sisi ni wenyeji na wakulima wa mahindi na tunajidai kwa sababu tunalisha mikoa mbalimbali yenye shida ya chakula pamoja na nchi za nje, kwa hiyo tunamkaribisha mama yetu kwenye mkoa wetu wa chakula angalau atakapoondoka tutampatia na yeye mahindi akale nyumbani,"anasema Mbilinyi.

Upendo Mwakikapwa alisema wao kama wafanyabiashara, wamejipanga vya kutosha kupokea na kuhudumia ugeni utakaofika mkoani kwao katika kipindi chote cha tamasha na kwamba watahakikisha wanatoa huduma zote zitakazohitajika kwa ubora.

“Baada ya kupata taarifa kwamba Rais Samia atatembelea mkoani kwetu wakati wa tamasha la utamaduni, tulianza kujipanga na mpaka sasa naweza kuwahakikishia wageni wote watakaofika kwamba tuko tayari kuwapokea na kuwahudumia,”anasema Upendo.

“Na tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wageni wote watakaofika kwenye mkoa wetu wanapata sehemu za kulala bila shida, wanapata chakula na huduma nyingine muhimu zitakazohitajika, na tunaamini na sisi wafanyabiashara na mwananchi mmoja mmoja tutanufaika, kwa hiyo tunashukuru kwamba hizi pilika zilizopo kwa sasa kutokana na ujio wa Rais Samia inasaidia kukuza uchumi kwa wakazi wa mkoa huu.”

Upendo alimpongeza Rais Samia kwa kazi ambayo ameifanya katika mkoa wao huo wa Ruvuma katika nyanja mbalimbali ikiwamo uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambayo imerahisisha kwa kiwango kikubwa ufanyaji wa biashara na kuchochea kukuza uchumi wao.

Alisema tofauti na miaka ya nyuma, kwa sasa mkoa huo unazidi  kukua kiuchumi kutokana na shughuli nyingi zinazofanyika humo ikiwamo zile za uchimbaji wa makaa ya mawe ambao umesababisha pia shughuli za usafirishaji kuongezeka.

“Kwa hiyo hata Rais akija atashuhudia hizi pilika zilizopo na kikubwa tunamshukuru sana kwamba amechangia kwa kiwango kikubwa shughuli za kiuchumi kuongezeka katika mkoa huu kwa sababu ya kuimarisha miundombinu ya barabara, na hata viongozi wanapofika namna hii, fursa zinaongezeka zaidi,”anasema Upendo.“

Alisema wafanyabiashara wote wa mkoa huo, wanafurahia ujio wa Rais Samia na wamepanga kumwambia neno la shukrani kwa mambo ambayo amewafanyia.

“Kwa hiyo ujio wa Rais Samia sisi tumeupokea kwa furaha kubwa, ni mkubwa kwa sababu utatuachia fursa kubwa, kitendo cha watu kusafiri kutoka sehemu mbalimbali na kuja katika mkoa wetu, sisi tunatakiwa tujiongeze, kutoka moyni mwangu mimi kama mwanamke, ninamkaribisha sana Rais wetu na wanawake wa mkoa huu tupo tayari kumpokea na hii ni neema kwetu,”anasema Upendo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments