WILAYA 106 ZAUNGANISHWA KWENYE MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

 



Mkurugenzi wa Ufundi na Undelezaji kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL,Mhandisi Cecil Francis ameeleza kuwa wamefanikiwa kuunganisha wilaya 106 katika mkongo wa Taifa wa Mawasiliano  Tanzania Bara kati ya Wilaya 139.

Hayo yamejiri katika ufunguzi wa kongamano la Connect2Connect lililofunguliwa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa,na limewakutanisha wadau wa mawasiliano wa ndani na nje ya nchi.


Amesema kuwa wilaya 33 ambazo bado hazijafikiwa na mkongo wa taifa wa mawasiliano,mwaka huu wa fedha wa 2024/2025,serikali imeshatenga bajeti ya kwenda kukamilisha shughuli hiyo,ili kuhakikisha wilaya zote zinaunganishwa na zianze kupata huduma bora.

Alisema mkongo wa mawasiliano wa taifa ni kiungo kikuu cha mawasiliano ya sauti na Intaneti ambapo inaunganishwa na mikongo ya baharini ambayo inaleta Intaneti nchini.

“Mkongo wetu wa taifa wa mawasiliano ni kiungo kikuu cha mawasiliano ya sauti,lakini vilevile na Intaneti na tunaunganisha na mikongo ya baharini ambayo inatuletea Intaneti hapa nchini na sisi pia tunaunganisha na nchi za jirani za Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi,Zambia na Malawi.

“Tunamaunganisho yamekwenda mpaka Msumbiji na tumeanza kuingia maunganisho yatakayofanya tuingie hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),kupitia Ziwa Tanganyika.alisema Mkurugenzi huyo wa Ufundi”

Pia alisema shirika hilo,linaendelea kuboresha maunganisho ya mkongo kwa kusogeza kwenye vituo vya baharini vilivyoko Mombasa nchini Kenya.

“Kazi kubwa tuliyonayo TTCL,ni kuhakikisha tunatoa mchango wa mawasiliano kwa mkongo tunayojenga inafika kila sehemu ikiwa na ubora wa hali ya juu kwa ajili ya kufikisha huduma kwa wananchi na kupunguza gharama za matumizi,”alisema.

Alisema shirika hilo,kupitia mkongo wa taifa wa mawasiliano wamefanya kazi ya kuunganishwa kwa mawasiliano mikoa kwa mikoa na wilaya kwa wialaya.

“Sisi TTCL,tukiwa kama chombo cha serikali tumepewa dhamana ya kutoa huduma za mawasiliano hapa nchini,”alisema.  

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Helios towers,Gwakisa Stadi,alisema kampuni hiyo kwa hapa nchini inasimamia minara zaidi ya 400 na wana wateja zaidi ya 10000 ambao ni watumiaji wa minara hiyo.

Alisema kazi kubwa ya mirana hiyo,ni kuunganisha huduma za mawasiliano na wateja wao wakubwa ni makampuni ya simu,kampuni za usambazaji wa Inteneti na televisheni zilizoweka vifaa vyao vya mawasiliano kwenye minara hiyo.





Previous Post Next Post