WADAU WAKUMBUSHWA KUSAJILI MASHIRIKA YAO


Na Bora Mustafa -Misalaba Media, Arusha

Wadau wa Mashirika yasiyo ya kiserikali wamekumbushwa kusajili mashirika yao ili yaweze kutambulika kisheria pamoja na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.

Hayo yamesemwa na Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Fatuma Amiri, na kusema kuwa teknolojia imerahisisha mambo mengi hivyo mambo yote yanafanywa kidigitali.                                                                            

"Asasi za Kiraia zina mchango mkubwa nchini, na zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuinua uchumi wa wananchi na kuboresha huduma za jamii" ameeleza Fatuma.

Ameongeza kuwa AZAKI  imesaidia kuinua vikundi vya akina mama nchini kuwapa elimu ya kukopa na kukopeshana, elimu  ya ukatili na uzazi bora. 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Haki elimu Mwemezi Makumba, amesema takwimu zinaonyesha kuwa ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya demokrasia ni mdogo. 

Ameeleza kuwa ni asilimia ndogo ya vijana wanaoweza kujieleza, kujinadi na kutetea haki zao, licha ya wengi wakifahamu vizuri juu ya kuheshimu haki za binadamu na utu wa mwanadamu. 

"Kwa tafiti hizi ni wazi vijana wanatakiwa kuamka na kutambua nafasi zao juu ya mchango wa maoni na hoja za kujenga nchi katika Dira ya Taifa ya 2050 ili kuifikia Tanzania tuitakayo" amesema Mwemezi. 

Hata hivyo Kijana kutoka  Wilaya ya Mbeya Tunsume Vibweji katika kigoda cha vijana amesema Vijana hawashirikishwi ipasavyo kwa maana ya kuwafikia walioko vijijini na kuzingatia makundi maalum bali ni maoni ya wachache huchukuliwa hali inayodhoofisha maono ya vijana wengi. 

"Mfano mimi kijana ninayeishi mjini na kutembelea mitandao ya kijamii kila wakati sipati nafasi ya kushirikishwa katika masuala ya kidemokrasia na mengine mengi ya kujenga taifa, hofu yangu ni juu ya vijana walioko vijijini kwamba hawana nafasi ya kujieleza wala kutetea hoja zao.

"Kutokana na changamoto hii, naomba kuishauri serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali iangalie kwa kina vijana waishio vijijini" amefafanua Vibweji.

 

Previous Post Next Post