Na Mapuli Kitina Misalaba
Jumla ya wanafunzi 45,693 mkoani Shinyanga
wanatarajia kuanza mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kesho, huku Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga, Anamringi Macha, akionya vikali dhidi ya udanganyifu katika
mitihani hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
Septemba 10, 2024, Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa mtihani wa darasa la saba
utaanza kesho na kumalizika kesho kutwa, ukihusisha wavulana 19,528 na
wasichana 26,165.
Ameongeza kuwa serikali haitasita kuchukua
hatua kali kwa shule, hususan za binafsi, zitakazobainika kujihusisha na
udanganyifu wa mitihani.
"Shule
za binafsi mara nyingi zinakuwa na ushindani mkali wa kutaka wanafunzi wafaulu
ili kupata sifa, lakini sitaruhusu udanganyifu wa aina yoyote shule
itakayokutwa inafanya udanganyifu itafungiwa mara moja," amesema Macha.
Ameonya pia shule za serikali, walimu, na
wazazi kutojihusisha na udanganyifu ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa
wanafunzi kuonyesha kile walichojifunza ndani ya miaka saba badala ya kusaidiwa
kwa njia zisizo halali.
"Walimu
na wazazi wasiwadanganye watoto, na wazazi pia wasiwashawishi watoto kufanya
vibaya kwa nia ya kuwaoza au kuwafanya wachungaji wa mifugo," amesisitiza.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa ameweka wazi kuwa
maandalizi ya mitihani yamekamilika, na walimu 3,339 wamepangwa kusimamia
mitihani hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba, akiwemo Mariamu Amosi kutoka shule ya msingi Mwenge, wamesema wako tayari kwa mitihani hiyo na wana matumaini ya kupata matokeo mazuri.