Watu watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama kwa kosa la kuhujumu uchumi kwa kuunda genge la uhalifu na wizi wa nyaya za umeme aina ya Alminiam zenye thamani ya Sh.milioni 54.
NA NEEMA NKUMBI - KAHAMA
Wakisomewa mashtaka hayo septemba 12, 2024 na Mkuu wa Mashtaka Ofisi ya Kahama, Jukaeli Jairo aliiambia mahakama kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Septemba tatu mwaka huu katika miji ya Kahama na Dar es Salaam ambapo walikutwa na gram tatu za nyaya ya Almininu.
Jairo amesema, watu hao wanakabiliwa na makosa mawili, kosa la kwanza ni kuunda genge la uharibu kwa makusudi kinyume na sheria 4(1)(a) inayosomwa pamoja na sheria namba 57(1) na 60(2) ya sheria ya uhujumu uchumi, huko kosa la pili likiwa ni wizi kinyume na kifungu cha sheria namba 258(1)(2)(a) na 265 ya kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Aidha amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na; Erick Kamuhanda Rweyemamu(36), Kaijage Kagenyi(27),Carlos Eck Chamanga(29), Ngwea Mkomwa Sufian(29), Lemi Paul Mtwale(34) wote wakiwa ni mafundi umeme pamoja na Rotan Eliezer Nzowa(38) Mkandarasi wa umeme.
Kesi hiyo namba 26208/2024 ilisikilizwa na Hakimu Mkazi mwandamizi wa Wilaya ya Kahama Edmund Kente na mzigo iliyoibiwa ilikuwa mali ya Iddcon Investment Limited aliyekuwa akitekeleza mradi wa Rea katika kata ya Idahina Halmashauri ya Ushetu.
Watuhumiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote katika kosa la kwanza na kosa la pili walikana mashtaka ambapo waliiomba Mahakama dhamana lakini dhamana ilishindikana kwa kuwa mahakama haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo la Uhujumu uchumi na kesi itatajwa tena septemba 27 mwaka huu.