WATANZANIA WATAKIWA KUJIUNGA NA HUDUMA ZA BIMA

Na Neema Kandoro Mwanza

WATANZANIA wametakiwa kujiunga na mifuko ya bima ili kujihakikishia usalama wa mali zao pindi majanga mbalimbali yanapotokea ghafla na kuathiri shughuli zao za kila siku.

Wito huo umetolewa jana jijini Mwanza wakati wa kilele cha maonesho ya biashara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyoandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani hapa.

Meneja wa Shirika la Bima Kanda ya Ziwa, Stella Marwa, aliwasihi wananchi kutumia mifuko hiyo kwa kuwa ina manufaa makubwa.

Alifafanua kuwa mifuko ya bima huwapa walaji nafasi ya kufidiwa endapo wataathiriwa na majanga, huku ikiwapa bonasi na faida mwishoni mwa mkataba wa bima.

“Bima ya Maisha ni mkataba kati ya mteja na kampuni ya bima, ambapo mteja anafidiwa kulingana na thamani aliyochangia endapo atapatwa na janga au kifo ndani ya muda wa mkataba”,  alisema Marwa.

Aliongeza kuwa bima hiyo hutoa akiba pamoja na faida mwishoni mwa mkataba, endapo mkataba utamalizika bila tatizo lolote.

Marwa alieleza kuwa bima ya maisha ni ya miaka 10 na inampa mteja au wategemezi dhamana ya kifedha, huku ikitoa bonasi ya asilimia 5.5 kila mwaka kuanzia mwaka wa pili wa uchangiaji.

Alisema zipo bima za aina nyingi hapa nchini zinazosaidia kufidia majanga yasiyotarajiwa, kama matetemeko ya ardhi, moto, vimbunga, na mafuriko.

“Ni muhimu kwa wananchi kukata bima kwa kuwa majanga haya yanaweza kujitokeza bila taarifa na kuwa na madhara makubwa,” alisema.

Alihimiza wananchi kutoa kipaumbele kwa bima kwani matukio yasiyotarajiwa yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mtu ambaye hana kinga ya kifedha.

Juma Adolph, mkazi wa mtaa wa Ghana, jijini Mwanza, alisema kuwa hakujua umuhimu wa bima, lakini baada ya kupata elimu hiyo mwezi Oktoba mwaka huu, ataanza kuchangia kiasi cha shilingi 5,000/- ili apate bima ya maisha







Previous Post Next Post