Na Mapuli Kitina Misalaba
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohammed Bashe, ameweka wazi mipango na hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo ili kuboresha sekta ya kilimo, hususan katika mkoa wa Shinyanga, ambao una mchango mkubwa kwenye uzalishaji wa mazao muhimu nchini.
Waziri Bashe ameyasema hayo katika ziara yake Mkoani
Shinyanga, wakati akizungumza kwenye kikao ambacho kimehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo wakuu wa Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, maafisa kilimo
pamoja na wafanyabiashara wa mazao Mkoani Shinyanga.
Sekta ya kilimo ni nguzo kuu ya uchumi wa Tanzania,
ambapo mwaka 2022 ilichangia asilimia 26.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) ambapo kilimo
kinatoa asilimia 65 ya malighafi za viwanda na kutoa ajira kwa asilimia 65.6 ya
Watanzania (NBS, 2020), huku kikiwa chanzo cha asilimia 30 ya fedha za kigeni
zinazopatikana nchini.
Waziri Bashe ameeleza kuwa serikali imejipanga
kusimamia kilimo-biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambayo ni mdau
muhimu katika kukuza sekta hii.
Amesema mchango wa teknolojia na utafiti wa kisasa
unaendelea kupewa kipaumbele, sambamba na kuhakikisha kuwa sera na sheria
zinalinda ardhi ya kilimo na kuimarisha mifumo ya masoko.
Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuwa na mchango mkubwa
katika uzalishaji wa mazao mbalimbali, lakini bado kuna changamoto za kuongeza
tija kwa mujibu wa Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao Wizara ya Kilimo Bwana
Nyasebwa Chimagu amesema Mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya 15 kati ya mikoa
26 kwa uzalishaji wa nafaka, ambapo unalimwa hekta 341,042 na kuzalisha tani
465,180.
Kwa mazao yasiyo ya nafaka, Shinyanga inashika
nafasi ya 18, ikilima hekta 211,012 na kuzalisha tani 239,021 hata hivyo, tija
ya mazao kama mahindi na mchele inabaki chini ya wastani wa kitaifa.
Mahindi huzalishwa kwa tani 1.3 kwa hekta, na mchele
kwa tani 1.4, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuzingatia matumizi ya kanuni
bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuyafikia masoko ya ndani na nje kwa
ufanisi zaidi.
Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao Wizara ya Kilimo
Bwana Nyasebwa Chimagu amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2024/2025,
wizara hiyo imepanga kuongeza nguvu katika maeneo yafuatayo:
Kuongeza
tija na uzalishaji – Serikali itaendelea kuhamasisha
matumizi ya teknolojia bora na kuongeza upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
Kuongeza
ajira kwa vijana na wanawake – Serikali inalenga
kuongeza ajira zenye staha kupitia kilimo, kwa kuhamasisha ushiriki wa vijana
na wanawake.
Kuimarisha
usalama wa chakula na lishe – Lengo ni kuhakikisha
uzalishaji wa mazao unakidhi mahitaji ya chakula nchini.
Kuimarisha
masoko na mitaji – Upatikanaji wa masoko na mitaji
utaendelea kupewa kipaumbele, ili kuimarisha usafirishaji wa mazao nje ya nchi
na kuongeza mapato ya wakulima.
Kuimarisha
ushirika – Serikali itaendelea kuhamasisha
maendeleo ya vyama vya ushirika katika kilimo ili kuongeza ufanisi.
Matumizi
ya mifumo ya TEHAMA – Mfumo wa kidigitali utaimarishwa
ili kurahisisha huduma kwa wakulima na kukuza maendeleo ya sekta hii.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Anamringi Macha amesema serikali itaendelea kushirikiana na wakulima pamoja na
wadau wa mazao ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya Kilimo.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mazao Mkoa wa
Shinyanga Bwana Hassan Mboje amepongeza kwa ushirikiano wa serikali huku
akiiomba serikali kutatua haraka changamoto zilizopo.
Naye mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga amesema
zipo fursa mbalimbali katika zao hilo hivyo amewahimiza wakulima kuchangamkia
fursa zinazojitokeza.