Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MCHENGERWA ATOA MAAGIZO HAYA DART,AZINDUA MFUMO WA KISASA

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa ameiagiza Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha inatatua changamoto ya uhaba wa mabasi hayo kabla ya Desemba, mwaka huu na kuwakaribisha Watanzania kushiriki katika zabuni kwa Dar es Salaam.

Pia serikali imekuja na mwarobaini wa kudhibiti upotevu wa mapato katika mradi wa DART kwa kuzindua mfumo wa kisasa wa kukusanya nauli kutumia kadi janja.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kadi janja na mageti janja katika mfumo wa DART, Mchengerwa alisema mfumo huo utasaidia kuzuia udanganyifu na kuongeza mapato ya serikali huku akiagiza kadi hizo zianze kutumika mara moja.

“Ni kweli kuna changamoto ya mabasi Watanzania wanasubiri mabasi kwa njia ya Kimara uhitaji wa mabasi ni 170 na Mbagala ni 500 DART hakikisheni mabasi yanapatikana kabla ya Desemba mwaka huu na muwakaribishe Watanzania kushiriki zabuni waje kushirikiana na serikali katika uwekezaji,”alieleza.

“Niwapongeze DART kwa kujibu hoja za wananchi, uzinduzi wa kadi janja na kuachana na matumizi ya karatasi unaleta mapinduzi makubwa ya namna tunavyotaka kuwahudumia Watanzania katika usafiri wa Dar es Salaam, inakwenda kujibu hoja na kutatua changamoto za wananchi za kulipa nauli,”alisema

Alisema uzinduzi huo unatokana na maendeleo ya teknolojia ya ukusanyaji wa nauli kwa DART, ambayo inaufanya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kuwa katika kiwango cha juu kabisa.

“Ninatambua hapo awali wananchi walipata changamoto nyingi , ukisoma katika mitandao ya kijamii, kila mtanzania analalamika, wapo waliokuwa wanalalamika kuhusu nauli zao, wapo waliokuwa wakitoa fedha zikiwa nyingi kupata chenji inachukua muda mrefu na wakati mwingine kukosa, mfumo huu utajibu maswali yao kwa muda mrefu,” alisema.

Aliagiza upatikanaji wa kadi hizo kuwa rahisi bila changamoto na DART kuongeza ufanisi kila anayetumia mwendo kasi afurahie kuishi Dar es Salaam, huku serikali ikijipanga kwenda katika majiji mengine pindi changamoto zote zikitatuliwa.

Mchengerwa alimtaka Mtendaji wa DART na UDART kushirikiana kutatua changamoto hizo na kutekeleza suala la muda wa mabasi kukaa kituoni na kuwa wakali kwa watumishi wasiosikia kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwahudumia Watanzania.

“Hatamani mimi sifurahishwi kuona watu wakikaa kituoni muda mrefu na wakati mwingine mabasi yakiwapita bila kuwachukua hivyo naagiza changamoto hii itatuliwe,” alisema.

Aidha Mchengerwa aliwataka watendaji hao zinapotokea changamoto zitatuliwe mara moja kwani hataki kuona mabishano katika masula ya biashara, wasikae ofisini watoke kuwabaini wasiofanya kazi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Othman Kihamia alisema mfumo wa kukusanya nauli wa kisasa wa kutumia kadi janja utasaidia kuepuka kutumia mfumo wa karatasi au pesa mkononi na kupunguza foleni.

Alisema kadi hizo zina ubora tofauti na zinazotumia maeneo mengine kwani zina vitu vingi ambavyo mtu anaweza kutumia sio kulipa tu nauli.

“Mfumo huu uliojengwa na Wakala hii unafaida nyingi ikiwa kuondoa matumizi ya karatasi yanayochangia uchafuzi wa mazingira.

“Pili kuondokana na suala la usumbufu katika chenji kwani ukizingatia nauli sehemu nyingi ni Sh 750, hiyo sh.50 imekuwa ikileta usumbufu na muda mwingine haupatikani, pia hupunguza muda wa kupanga foleni kulipa nauli katika vituo vyetu,” alieleza.

Post a Comment

0 Comments