Na Elizabeth Zaya
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Damas Ndumbaro, ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), kuwashughulikia wale wote wanaohamasisha mmonyoko wa maadili kupitia mitandao ya kijamii na kusigina mila na tamaduni za Kitanzania.
Dk.Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua Tamasha la Kitaifa la Utamaduni mjini Songea mkoani Ruvuma.
Amesema hakuna taifa lolote duniani lisiloheshimu na kuthamini mila, desturi na tamaduni zao na kwamba ni jukumu la TCRA kuwashughulikia ipasavyo wale wote wanaotumia vibaya mitandao hiyo.
"TCRA mna jukumu kubwa la kuhahikisha wale wanaokiuka mila na desturi za Kitanzania, kuzisigina na kuhamasisha mambo yanayochangia kuleta mmonyoko wa maadili katika nchi yetu wanashughulikiwa ipasavyo,”amesema Dk.Ndumbaro.
“Tusipokuwa na utamaduni wetu, hatuna utu na tusipouenzi hatutauendeleza na ili taifa liwe hai lazima kuenzi na kuendeleza utamaduni wake, lazima turithishe utamaduni kwa vijana pamoja na watoto,tuwafundishe mila na desturi za Kitanzania, kiswahili, miiko yetu na ndipo taifa litaendelea kuwa hai.”
Amesema licha ya umuhimu mkubwa uliopo katika kuheshimu haki za binadamu, lakini wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya tafsri ya haki hizo za binadamu kuingiza tamaduni za kigeni ambazo ni kinyume na zile za Kitanzania na kwamba suala hilo halikubaliki.
"Haki za binadamu ni suala muhimu sana ambalo tunahitaji kuliheshimu na kulizingatia, lakini baadhi tunatumia haki za binadamu vibaya kwa kuingiza tamaduni za kigeni zisizofaa katika jamii yetu, tusitumie kisingizio hicho kukiuka miiko, maadili na desturi zetu kwa kuwa tukifanya hivyo tutakuwa tunaiua nchi yetu na kufanya hivyo nchi yetu itakuwa mfuu,”amesema Dk.Ndumbaro.
"Waswahili wanasema mkataa kwao ni mtumwa na sisi tusikatae kwetu, katika kuenzi mila na desturi lazima tutambue taasisi muhimu ambazo zinaweza kufanikisha jambo hilo tukianza na familia, taasisi za dini, vyombo vya habari, shule na nyinginezo.”
Amesema maadili mazuri ndio yatalisaidia taifa kuondoa mmonyoko wa maadili.
“Tunaamini kwamba taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kulinda maadili ya nchi yetu, watengeneza maudhui katika mitamdao ya kijamii na vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa, kwa hiyo ninavisihi vitusaidie katika hilo,”amesema Dk.Ndumbaro.
Dk.Ndumbaro amesema kaulimbiu katika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni mwaka huu inasema ‘utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza."
Kilele cha Tamasha hilo ni Septemba 23 mwaka huu na linatarajiwa kufungwa na Rais Samia.
Mwisho.