WEGS: KUKUZA UWEZO WA WASICHANA SHULENI NA MTAANI KANDA YA KASKAZINI


Mkurugenzi wa Shirika la Women Economy and Gender Support, Joyce Mwanga (wa mbele jukwaani) akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Kikwe iliyopo jijini Arusha.

Na Bora Mustafa, Misalaba Media, Arusha.

SHIRIKA la Women Economy and Gender Support (WEGS) limedhamiria kumuinua mtoto wa kike kitaaluma pamoja na stadi za maisha kupitia mradi wake wa Promote Potential for Adolescent Girls katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Mkurugenzi wa Shirika hilo Joyce Mwanga amesema mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara unaangalia uwezo wa mtoto wa kike kwani mtoto wa kike ana uwezo mkubwa lakini anashindwa kufikia malengo yake kutokana na mila potofu pamoja na mazingira duni hivyo mradi huo umekuja kuwasaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Akizungumza katika shule za secondari za Nduruma na Kikwe zilizopo wilayani Meru jijini hapa amesema wametoa elimu wanafunzi ya kutambua haki zao.

"Haki zao tulizowafundisha ni kujitambua, kujitetea pamoja na kujifunza stadi za maisha ili kumuandaa kuwa mwanamke mwenye malengo hapo baadaye, na leo tupo hapa Kwa ajili ya kuwapa motisha yaani kuwapongeza wale waliofanya vizuri na walioshiriki pia" amesema Mwanga.

Akitoa zawadi ya fedha taslimu kwa wanafunzi wa kike sita ambapo kila mmoja alipata kiasi cha shilingi 120,000 na wanafunzi wa kiume sita nao walipongezwa kwa kupewa kiasi cha shilingi 50,000 kila mmoja kutoka shule zote mbili ambao walifanya vizuri katika kujibu maswali pamoja na stadi za maisha, Mwanga amesema hatua hiyo iwe chachu kwao na kwa wanafunzi wengine kujituma ndani na hata nje ya shule ili kujiweka tayari katika kukabiliana na maisha hapo baadaye.

Mbali ya fedha taslimi, pia wanafunzi 48 wakipata vyeti vya ushiriki.

Aidha ameeleza kuwa katika mradi huo, hawajawaacha nyuma watoto makundi maalumu kama walemavu na kwamba wanawangalia wanapitia changamoto gani ili waweze kuzitatua huku akitoa wito kwa wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu kuwa wawapeleke shule Kwani na wao wana haki za kupata mahitaji kama watoto wengine .

Kwa upande wake Afisa Mradi huo Emmanuel Mwenera amesema lengo la kuwafundisha watoto stadi za maisha ni kuwasaidia watoto kufahamu kitu kitakachowasaidia hasa pale wanapomaliza kidato cha nne kwani wanafunzi wengi wakimaliza shule hukosa kitu cha kufanya.

"Zamani mashuleni kulikuwa na stadi za maisha ila kutokana na mtaala wa sasa hakuna tena stadi za maisha hivyo naiomba serikali kuangalia upya mitaala ya elimu na kuiboresha zaidi kwa sababu watoto wengi wanasoma sana masomo ya darasani kuliko masomo ya vitendo, hii itasaidia wakiwa mtaani waweze kujisimamia na kukubalika katika jamii" amesema Mwenera.

Mwenera amesema mradi huo umewasaidia watoto kujua ndoto zao na vipaji vyao na ili shule iweze kuwa na sifa za kujiunga na mradi huo inatakiwa kuwe na mhemko wa wanafunzi wengi .

Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la DKA nchini Tanzania, Austria Amina -Anna Niko amesema kuwa Shirika hilo linadhamini mashirika yasiyo ya kiserikali yenye malengo ya kuinua jamii hivyo ameeleza kuwa lengo la wao kuidhamini WEGS ni kuinua usawa wa kijinsia katika jamii hasa kwa mtoto wa kike .

Amesema mradi huu umekuwa na ubunifu mkubwa na lengo zuri la kuinua uwezo uliopo ndani ya mtoto wa kike kwani ni kundi linalokandamizwa na mifumo mbalimbali ya jamii.

"Changamoto wanazopitia watoto wa kike zinachangia kuwarudisha nyuma, pia jamii nyingi bado zina mila potofu juu ya mtoto wa kike hivyo ni furaha kubwa kuona WEGS wanampa elimu mtoto wa kike ili aweze kujipambania kutoka katika mifumo mbalimbali inayomkandamiza" amesema Niko 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la SASA Foundation, Jovita Mlay amewapongeza washiriki wa shindano hili kwa kuonyesha uthubutu na amewashauri wanafunzi wengine wawe na uthubutu kwenye kila fursa kwa kujitokeza kwani anaamini wote wana mawzo mazuri na wenye tija.

"Pia niwapongeze walimu wa shuleni zote kwa kuwa mmewawezesha watoto kuwa katika stadi za maisha, na kutokana na shindano hili kusahihishwa kwa usahihi wanafunzi walioshiriki nawapa nafasi ya kusoma masomo ya ziada wakati wa kumaliza kidato cha nne kwa muda wa miezi miwili na nusu katika sekta za upishi, ushonaji na upambaji" amesema Mlay.

Kwa upande wake mwanafunzi Ombeni Sifaeli amewapongeza waalimu kwa kuwajengea uwezo mzuri wa kujibu maswali ipasavyo na amewasisitiza wanafunzi waendelee kujibu maswali kwa kina hatua itayowasaidia  hata nje ya masomo.

Kwa upande wa Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Kikwe, Julius Sindato ameeleza  kuwa amefurahi  kushirika katika mradi huo kwa kuwa  umemuonyesha kujali na kuwasaidia wanafunzi wao kujitambua na kujua nafasi zao katika jamii .

Pia kwa wanafunzi ambao waliibuka washindi wamesema kuwa wamepata faraja na watatimiza ndoto zao walizoandika katika ushindani na iwapo fursa yoyote itatokea wataichangamkia.



Previous Post Next Post