WIKI YA AZAKI 2024 KUANZA KESHO JIJINI ARUSHA.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM  International Nesia Mahenge pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya ya wiki ya AZAKI 2024 akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha.


Na Bora Mustafa, Misalaba Media -
Arusha.

WIKI ya Asasi za Kiraia (AZAKI) inatarajiwa kufanyika kuanzia kesho Septemba 9 hadi 13 jijini Arusha.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM International Nesia Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya wiki ya AZAKI 2024 akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha.

Mahenge amesema kuwa kwa mwaka huu wiki hii ya AZAKI itawakutanisha watu zaidi ya 500 ambapo Kauli Mbiu ni "Voice, Vision and Value" (Sauti, Dira na Thamani).

"Wiki hii tunakutana kwa ajili ya kuzungumza kuhusu wiki ya AZAKI, tunaangalia changamoto na tunaangalia kama AZAKI na Serikali namna gani tushirikiane kwa ajili ya maendeleo," amesema Mahenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society Justice Rutenge amesema sababu ya kuwa na Kauli Mbiu hiyo kwa mwaka huu ni kutokana na kwamba tupo katika kipindi muhimu cha Demokrasia.

Kwamba mwaka huu baadaye kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa kukusanya maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 na mwakani Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Kuhusu Dira ya Taifa Rutenge amebainisha kuwa pamoja na tofauti tulizo nazo kama Watanzania mwisho wa siku Dira ni maoni ya Watanzania.

Kwamba kwa upande wa Thamani amesema ni muhimu kuwa na Utekelezaji wa Dira ya Taifa ili kifikia Maendeleo ya Taifa ambapo amebainisha kuwa katika Wiki ya AZAKI Thamani itapatikana kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

"Kutakuwa na ushiriki wa Serikali, Sekta binafsi, Sekta ya Umma, mashirika mbalimbali ya ndani na kimataifa na wananchi," amesema Rutenge.

Mkurugenzi wa Haki Elimu John Kalage amesema tafiti zinaonyesha ushiriki wa vijana Katika nyanja mbalimbali hususani kwenye masuala ya demokrasia ni hafifu hivyo kupitia wiki hii ya AZAKI vijana watapa fursa ya kutoa maoni yao juu ya ushiriki wao katika nyanja zote za maendeleo nchini.

"Tutawaleta vijana watazungumza ushiriki wao wa demokrasia ndani na nje ya shule kupitia kigoda cha vijana kwani wao wana nafasi mbili ambazo ni kuomba nafasi za uongozi pamoja na kushiriki mchakato wa kupata viongozi ambao wanaamini wanaweza kuwaongoza" alisema Kalage.



Ishmail Biro, Mkurugenzi Tanzania Bora Initiative
Previous Post Next Post