WIZARA ya Afya imeipatia Taasisi yaTaifa ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR) bilioni mbili kufanyia tafiti na kusaidia kuendeleza tiba asili ili ziweze kutoa michango mkubwa wa matibabu hapa nchini.
Haya yamebainishwa Leo kwenye kilele cha Kongamano la Prof Said Aboud akisema kutokana na mchango mkubwa wa tiba asili katika kupambana na maradhi kwenye jamii wameona ipo haja kubwa kwa sasa kufanyia tafiti dawa hizo ili ziweze kusaidia kwenye tiba za binadamu.
Alisema kutokana na tafiti mbalimbali walizofanya kwa sasa wameanza kusambaza tiba asili katika hospitali saba za Kanda ambapo dawa hizo zinaonesha matokeo chanya kwa matibabu ya maradhi mbalimbali.
Prof Aboud alisema kuwa washiriki 250 kutoka sekta tofauti wakiwemo waganga wa tiba asili,watafiti wa magonjwa ya binadamu na watunga sera wameshiriki katika Kongamano hilo liloanza tatehe 25 na kuhitimishwa Leo.
Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin mollel aliitaka jamii kuondoa unyanyapaa dhidi ya tiba asili hivyo aliitaka NIMR kuendelea kusaidia kufanya tafiti kubwa ili dawa hizo ziwe na sura ya tiba za sayansi zingine.
"Nawaomba NIMR fanyieni tafiti dawa hizo ili ziweze kuwa bora zaidi na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kupambana na magonjwa kama mlivyofanya kipindi kile cha ugonjwa UVIKO19" alisema Dk Mollel.
Alisema serikali Iko bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa tiba hizo zinafikia malengo ya kutoa huduma nzuri na za kutumainiwa na watanzania na sehemu zingine nje ya nchi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili wa Wizara ya Afya Prof Hamis Malebo alisema kuwa wameshasajiri zaidi ya Waganga Tiba Asili 54,000 na dawa zao Zina ufanisi na zimeonesha kuwa na mafanikio makubwa ambapo zimeanza hata kusambazwa nje ya nchi.
Alisema wanachoendelea kufanya ni kuwajengea elimu waganga wa tiba asili juu ya umuhimu wa kuzifanya tiba hizo kuwa bora na zenye ufanisi kwa kushirikiana na NIMR.