Na Mapuli Kitina Misalaba
Katika jitihada za kuimarisha demokrasia na ushiriki
wa wananchi katika maendeleo, Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Shinyanga kimetangaza rasmi kuwa kimesimamisha
wagombea katika mitaa yote kwa ajili ya nafasi za uenyekiti.
Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Shinyanga, Omary
Gindu, amesema kuwa chama chake kimejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanapata
viongozi wanaoendana na matakwa yao ya maendeleo.
Akizungumza
leo na Misalaba Media, Gindu ameeleza kuwa lengo la chama hicho ni kutoa
viongozi bora watakaosimamia haki na maslahi ya wananchi, badala ya kufuata
itikadi za kisiasa pekee.
“Uchaguzi
huu siyo wa kufurahisha vyama bali ni wa kuhakikisha wananchi wanapata viongozi
watakaowaletea maendeleo, wananchi wanayo nafasi ya kufanya maamuzi sahihi ili
kuboresha maisha yao kupitia uongozi unaojali jamii”.amesema
Gindu
ACT Wazalendo inaendelea na kampeni zake za kutoa
elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
uchaguzi na kufanya maamuzi yatakayosaidia kujenga mustakabali bora kwa vizazi
vijavyo.
Kwa upande wake katibu wa ACT Wazalendo jimbo la Shinyanga Mjini Juster
Denis, amesema chama hicho kimefanikiwa kukamilisha zoezi la kurudisha fomu kwa
wagombea wa mitaa yote katika kata sita, huku kata zingine zikitarajiwa
kurudisha fomu zao kesho, Ijumaa Novemba 1, 2024.
Juster ameeleza kuwa zoezi la kuchukua na kurudisha
fomu limekwenda vizuri ndani ya chama hicho, ambapo wagombea wamefuata taratibu
zote zilizowekwa na chama.
"Zoezi limekuwa salama na kila mgombea
ameweza kujaza fomu kwa utaratibu sahihi, tukithibitisha umakini wa chama
katika kuhakikisha wagombea wanatekeleza wajibu wao kwa uwazi na haki,"
amesema Juster
"Tumewasimamisha wagombea wetu katika mitaa
yote, na leo tumerejesha fomu za wagombea kutoka kata sita, ambazo ni Ndembezi,
Ngokolo, Kambarage, Masekelo, Mwawaza, na Kizumbi," amesema Juster.
Hata hivyo, Juster amegusia changamoto iliyojitokeza
kuhusu fomu za wagombea akifafanua kuwa kanuni za chama hazijaelekeza kwamba
wagombea watoe picha za passport, lakini katika baadhi ya maeneo wagombea
walitakiwa kuweka picha hizo.
"Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu kwa
wagombea limekwenda vizuri, na tunashukuru kwa kukamilika salama ingawa
kulikuwa na changamoto ndogondogo, kama vile baadhi ya maeneo kuwalazimisha
wagombea wetu kuweka picha za passport, jambo ambalo halipo katika kanuni
zetu," amesema Juster.
"Hali hii inatupa mashaka kidogo, kwani tunaona fomu za wagombea wa CCM zilipelekwa kujazwa sehemu moja tunauliza, kwa nini zimekusanywa mahali pamoja? Je, lengo ni kuandaa pingamizi dhidi ya wagombea wetu, au pengine wale wagombea waliowasimamisha hawajui kusoma na kuandika? Tunajiuliza kwanini fomu zao zikusanywe na kujazwa pamoja au wagombea ambao wamewaweka hawajui kusoma na kuandika" amesema Juster.
Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Shinyanga, Omary
Gindu, akizungumza na Misalaba Media leo Oktoba 31, 2024.
Katibu wa ACT Wazalendo jimbo la Shinyanga Mjini Juster Denis, akizungumza na Misalaba Media leo Oktoba 31, 2024.